13 July 2011

Wabunge wampania Waziri Ngeleja

Na Waandishi Wetu, Dodoma

WAKATI bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ikitarajiwa kusomwa Ijumaa wiki hii, dalili zimeanza kujitokeza baada ya wabunge wengi kuonesha shauku ya kuchangia
mjadala huo kutokana na mgawo wa umeme nchini.

Hali hiyo ilidhihirika jana wakati wa kipindi cha maswali na majibu baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Bi. Jenista Mhagama kumpa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza mbunge wa Mtambile, Bw. Masoud Abdallah Salim, aliyetaka kujua serikali inawaambia nini Watanzania juu ya ufumbuzi wa tatizo la umeme ambalo linaendelea kuathiri maisha ya Watanzania na taifa kwa ujumla.

Miongoni mwa wabunge hao ni mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe ambaye alipopewa fursa ya kuuliza swali la nyongeza, alisema anashindwa kuelewa kwanini serikali haisemi lolote kuhusu tatizo la umeme, na baadaye baadhi ya wabunge walionesha nia ya 'kumkaba koo' waziri huyo wakati wa bajeti yake.

Bw. kabwe alisema tatizo hilo linatokana na mashine za kampuni ya Pan African kupata kutu.

Pia, alisema tangu tatizo hilo lilipoanza Mei mwaka huu, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imepoteza zaidi ya sh bilioni 800 na kuhoji ni kwa nini mpaka sasa Waziri wa Nishati na Madini, Bw. William Ngeleja na naibu wake, Bw. Adam Malima hawajajiuzulu.

“Suala la umeme ni kizungumkuti, lakini kuna tatizo la serikali kutosema ukweli kwa wananchi. Tatizo ni kutu zilizopo kwenye mashine,” alisema.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Adam Malima, alisema tatizo si visima vya kufulia gesi bali ni mashine za Pan African kuwekwa kemikali ambazo zilisababisha mashine hizo kuwa na kutu.
 
Alisema walidhani kuwa mashine hizo zingeweza kudumu kwa miaka 12, lakini zimeharibika kutokana na kemikali.

Akijibu swali la msingi la Bw. Salim, Naibu Waziri huyo, alisema ni kweli kwamba nchi imekumbwa na tatizo la umeme linalotokana na uwekezaji mdogo usiolingana na ukuaji wa mahitaji kwa muda mrefu.
 
“Hata hivyo, nchi yetu ina rasilimali nyingi ambazo zote zinaweza kutumika kuzalisha umeme ili kuondokana na tatizo la ukosefu wa umeme na serikali ina mipango mbalimbali ya muda mrefu na muda mfupi ya kukabiliana na tatizo hilo na katika kipindi cha muda mfupi, serikali inajielekeza kupambana na tatizo hilo kwa kuharakisha upatikanaji wa mitambo iliyokusudiwa kununuliwa ya megawati 100 Dar es Salaam na megawati 60 Nyakato, Mwanza na hatua za kununua pamoja na kuifunga mitambo hiyo zinatarajiwa kukamilika Aprili mwaka kesho,” alisema.
 
Alisema kuwa hivi sasa upungufu wa umeme unakadiriwa kuwa megawati  260 kwa sababu ya kukua kwa mahitaji ya umeme na kwamba mitambo hiyo itakapofungwa kutakuwa na nakisi ya megawati 100 na nyongeza itakayotokana na ukuaji wa mahitaji yanayokua kila siku.
 
Bw. Malima alisema kuwa serikali imelielekeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kusimamia utaratibu wa kukodi mitambo Machi mwaka huu, ili kufidia uhaba wa megawati 260 uliopo sasa, na shirika hilo limekamilisha makubaliano ya kukodi mitambo ya megawati 100 mwishoni mwa Juni, mwaka huu.

Wakizungumza na Majira nje ya bunge baadhi ya wabunge walisema wakati wa mjadala wa bajeti hiyo, watamtaka waziri huyo kueleza kila kitu kinachokwamisha umeme kupatikana hadi mgawo wa umeme kuendelea kila mwaka bila kupata suluhisho.

3 comments:

  1. atakoma na kuujua uchungu wa cheo

    ReplyDelete
  2. Only a STUPID person will believe on CCM MPs.

    Count my words CCM MPs will pass/agree with the energy budget by 100%

    ReplyDelete
  3. Kwa hakika kwa mahesabu ya megawati watu wa wizara ya Nishati na Madini ni wataalamu sana. Kama alivyosema mbuge wa Musoma (M), Watanzania shida yetu ni umeme na siyo mahesabu ya megawati.

    Jamani inakera na kuaibisha sana. Wajibika Ngeleja kama umeshindwa kutuhakikishia watanzania umeme wa hakika sema, maana ulisema mgao wa umeme itakuwa historia Tanzania, kwa hakika umelidanganya taifa.

    ReplyDelete