Na Benjamin Masese
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro, imezindua kampeni ya kuwahamasisha Watanzania kujivunia umoja na mafanikio yaliyopatikana katika
kipindi cha miaka 50 ya uhuru.
Uzinduzi huo ulifanyika Dar es Salaam jana katika Makumbusho ya Taifa huku yakianishwa mambo sita ya kujivunia ikiwa ni pamoja na amani, kiswahili, heshima na ukarimu, rasilimali na umaarufu wa kuwaheshimu na kuwaenzi watu walioiletea Tanzania sifa katika maeneo tofauti.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Bw. Robin Goestzche alisema Desemba 9, mwaka huu Tanzania inatimiza miaka 50 tangu kupata uhuru wake hivyo kampuni hiyo imechukua jukumu la kuungana na serikali kuwakumbusha kujitathmini walikotoka na wanakokwenda.
Bw. Goestzche alisema katika kuelekea mwishoni mwa kampeni hiyo ya iliyobatizwa 'Kili Jivunia Utanzania' kutakuwa na mbio za kupeperusha bendera ya Taifa zikijumuisha wanariadha mbalimbali kutoka mikoa minne na kumalizikia katika lango la Mweka wilaya Moshi.
Alisema baada ya wanariadha hao kukutana hapo bendera moja itapelekwa na kusimikwa kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro kama alivyofanya Marehemu Alexander Nyirenda kwa kusimika bendera ya Tanganyika na Mwenge wa Uhuru katika mlima huo.
Naye Mkurugenzi wa Masoko wa TBL, Bw. David Minja alisema kuwa kuanzia leo kutakuwa na matukio mbalimbali ya kuwahamasisha Watanzania wajivunie umoja wao na mafanikio walioyapata katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru.
No comments:
Post a Comment