15 July 2011

TANESCO yajipanga kumaliza tatizo la mgawo

Na Dunstan Bahai

MAKALI ya mgawo wa umeme katika mikoa mbalimbali nchini, huenda yakapungua baada ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO), kufunga mitambo mitatu ya gesi ambayo
itazalisha umeme wa megawati 100.

Mitambo hiyo yenye thamani ya dola za Marekani milioni 120 (zaidi sh. bilioni 120 za Kitanzania), ufungwaji wake utakamilika mwishoni mwa mwaka huu.

Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, baada ya kuwasili mtambo mmoja kati ya mitatu ambao unatarajiwa kuzalisha umeme wa megawati 34, Meneja Uhusiano wa shirika hilo Bi. Badra Masoud, alisema mitambo mingine iko njiani kuja nchini.

“Mitambo hii inatengenezwa nchini Sweden na Kampuni ya Siemens ambapo mafundi ambao wataifunga, watatoka Kampuni ya Umeme Jackobsen nchini humo,” alisema.

Akizungumzia mgawo wa umeme unaoendelea, Bi. Masoud alisema haufuati ratiba kutokana na masuala ya kitaalamu.

“Unaweza kukuta bwawa moja linalozalisha umeme halina maji ya kutosha hivyo huwezi kuwasha mashine kwani kufanya hivyo ni kuziua, katika hali ya kawaida baadhi ya maeneo yatakosa umeme.

“Katika mitambo yetu ya gesi, kama msukumo wa gesi ukipungua ni wazi kuwa umeme katika gridi ya Taifa utakuwa na hitilafu,” alisema na kuongeza kuwa, mitambo hiyo itasaidia kupunguza makali ya mgawo ambapo tayari wamewasiliana na Serikali ili iwasaidie mafuta ambayo watayatumia kuwasha mitambo ya IPTL.

“Sijajua kiasi gani cha fedha kitagharimu mafuta haya wala idadi yake lakini mazungumzo yanaendelea kati yetu na Serikali, mgawo huu hauwaathiri wafanyabiashara pekee bali Watanzania wote kwa ujumla, sisi kama shirika pia tumeathirika kwa kiasi kikubwa,” alisema.

Bi. Masoud alisema jamii imekuwa ikikosa imani na shirika hilo ingawa hali halisi inajulikana kwamba matatizo yanayotokea si uzembe bali ni masuala ya kitaalamu zaidi.

6 comments:

  1. Uamuzi wa serikali au Tanesco kununua mitambo ya kuzalisha umeme ulitakiwa kufanyika muda mrefu uliopita lakini kwa sababu ya 10% mambo hayo yalishindikana kufanyika kwa sababu ya uroho wa pesa kwa viongozi walio madarakani.Hiki ndio kilichotakiwa kufanyika na sio kutegemea mitambo ya kukodisha kila siku.Pia kuna nchi kama Brazili wao wanamitambo ya kuzalisha umeme inayotumia takataka ambazo zinazalisha gesi ambayo inazalisha umeme.Hapa ni kazi tu ya serikali kuwa na magari ya kutosha ya kusomba takataka zote na kwa maana nyingine inasaidia kuweka jiji katika hali ya usafi pamoja na kuwapatia wananchi kazi kwani huu ni mradi wa kudumu na hauna gharama kubwa za mafuta ya kuendesha mitambo.Viongozi wanatakiwa kuangalia wenzetu waliondelea wanafanyaje miradi yao na sio kuishia kula 10%.

    ReplyDelete
  2. Yaani wewe mwandishi sio analytical kabisa...yaani unasombwa na propaganda ya serikali kuhadaa watanzania kwamba matatizo ya umeme yataisha.....I wish ungekuwa na maono...kutambua kwamba hii ni hujuma inayofanywa na watawala

    ReplyDelete
  3. Tanzania imejaa hujuma hii, ni kweli kabisa, wanamuhujumu rais, wafuatiliwe hawa

    ReplyDelete
  4. Nanukuu "Bi. Masoud alisema jamii imekuwa ikikosa imani na shirika hilo ingawa hali halisi inajulikana kwamba matatizo yanayotokea si uzembe bali ni masuala ya kitaalamu zaidi." SIO KWELI KABISA... KINACHOTUGHARIMU NI MIKATABA MIBOVU ISIYO NA UALISIA NA MATUMIZI MABAYA YA RASILIMARI ZA NCHI. UFISADI... ilikua Richmond, ileile ikawa Dowans, leo imebatizwa inaitwa Symbion. vichekesho

    ReplyDelete
  5. I Love what I am reading here because the problem is the faithful citizen taking every crap from the politicians, corporate, firms, businessmen/women and life goes on and this is the only reason whey they take advantage of us (citizen) We will be humiliated, subjected to unnecessary suffering till when we wake-up and declare enough is enough. I will start with my right to VOTE.

    ReplyDelete
  6. Naunga mkono hapo juu... ni vichekesho kweli, Richmond, dowans, Symbion n.ke. yaani bora ya Somalia amboko mtu unaweza kusema hakuna serikali kwa hiyo "its okay" kama vili nchi imejaa mazezeta jamani hii sio kweli jamaaaaniii watu wa america watasema.... "IS THIS FOR REAL?"

    ReplyDelete