15 July 2011

Kawambwa aikabidhi mikoba bodi ya mikopo elimu ya juu

Na Rehema Mohamed

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa, amewataka Wakurugenzi wa Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu, kuacha kubweteka na kufanya
kazi kwa mazoea ili kukabiliana na changammoto zinazoikabili bodi hiyo.

Dkt.Kawambwa alitoa kauli hiyo Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya wakurugenzi iliyokabidhiwa majukumu yake jana.

Dkt. Kawambwa alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na bodi hiyo kushindwa kukusanya malimbikizo ya madeni ya mikopo inayoitoa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Dkt.Kawambwa alisema bodi kutokukusanya marejesho ya mikopo iliyotolewa inadumaza uwezo wa utowaji wa mikopo hiyo, huku idadi ya wanafunzi wanaoihitaji ikiongezeka kila mwaka.

"Kuna kazi kubwa mbele yenu ambayo inahitaji majibu ya haraka, kwa mfano ,bodi kutokusanya marejesho ya mikopo iliyotolewa, hali  inayodumaza uwezo wa utowaji wa mikopo,"alisema Dkt. Kawambwa.

"Nchi ya Kenya inakusanya asilimia 70 ya mikopo waliyokopesha huko nyuma,  wakati hapa nchini tunakusanya chini ya asilimia tatu tu ya kilichokopesha,kwa kukusanya kiasi hicho serikali ya Kenya huchangia asilimia 31 tu sawa na sh.bilioni 22 za Kitanzania kati ya bilioni 70 ya bajeti ya mwaka ya bodi ya nchi hiyo,"alisema.

Katika hatua nyingine aliitaka bodi hiyo kuwa na mikakati ya namna ya kukupunguza utegemezi kwenye chombo kimoja tu cha utowaji wa mikopo kwa wanafunzi nchini.

Kwa upandewake Mwenyekiti wa Bodi, Professa Anselm Lwoga, alisema bodi yake itajitahidi kutekeleza hayo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu sera ya uchangiaji elimu ya juu.

Prof. Lwoga alisema hatua hiyo itasaidia maendeleo ya mfuko wa bodi ili iweze kutoa mikopo kwa wanafunzi watakaokuwa na vigezo vya kukopeshwa.

Wajumbe wengine katika bodi hiyo ni Prof. Abeli, Bw. David Kazuva, Bi. Monica Mwamunyange, Bw. Omar Omar, Prof. John Shao, Prof. Salome Misana, Bw. Leonard Kisarika, Bi. Winfrida Koroso, Bi. Bertha Minja, Dkt. Musa Assad, Prof. Sifuni Mchome, Bi. Dina Mori na Bw. Mohamed Abubakar

1 comment:

  1. Kwambwa umesema mambo mazuri kabisa, lakini wakati hayo yakiendelea jua kuwa wapo mamia ya watanzania binafsi wamekwama kufanya mtihani wa kidato cha sita kutokana na sababu kadha wa kadha...hasa ukosefu wa umeme wa uhakika, kutokuwa na knowledge ya kutosha ya kutumia teknohama na kwa taarifa yako hata kazi kadha waka kadha zimekuwa zikikwama pale Baraza la Taifa la Mtihani kutokana na tatizo la umeme.

    Sasa watahiniwa hao wanalia wakiomba angalau wapatiwe wiki oja ili wajisajili..... lakini Mkuu Kawambwa kufunga usajili wa mtihani unaotarajiwa kufanyika miezi minane baadaye ni HAKI? wasaidiwe kama ni msaada........

    ReplyDelete