06 July 2011

Simba yaizima Bunamwaya

*Kuivaa El Mereikh kesho

Na Zahoro Mlanzi

'CCM', 'CCM', 'CCM', ndivyo ilivyosikika kwa mashabiki wa Simba wakiishangilia timu yao baada ya kutinga nusu fainali ya mashindano ya Kagame Castle Cup, baada ya
kuichapa Bunamwaya ya Uganda   mabao 2-1.

Shangwe hizo zilianza kwa nguvu baada ya kiungo Jerry Santo kuifungia bao la ushindi timu yake dakika ya 83,  akiunasa mpira uliookolewa na mabeki wa Bunamwaya kutokana na shuti lililopigwa na Ulimboka Mwakingwe kuzuiwa na mabeki wa timu hiyo.

Hakika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia dakika hiyo, ulitawaliwa na vifijo na nderemo zilizotokana na maelfu ya mashabiki wa Simba waliokuja kuishangilia timu yao katika mashindano hayo.

Kwa ushindi huo wa jana, Simba itaumana na El Merreikh ya Sudan katika mechi ya nusu fainali ya kwanza itakayopigwa kesho kwenye uwanja huohuo.

El Merreikh imetinga hatua hiyo kwa kuiondoa Ulinzi ya Kenya kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 9-8, mchezo uliopigwa saa nane mchana.

Katika mchezo huo wa Simba dhidi ya Bunamwaya, ulianza kwa kasi na kushambuliana, lakini Bunamwaya ilikuwa ya kwanza kupiga hodi langoni mwa Simba, baada ya Ronald Muganga kupiga krosi ambayo kama si Amir Maftah kuokoa na kuwa kona tasa, yangekuwa mengine.

Baada ya shambulizi hilo, Simba ilitulia na kushambulia kwa kushtukiza, ambapo dakika ya nane, beki Habib Kavuna akiwa katika harakati za kuokoa, alijikuta akiutumbukiza mpira wavuni kutokana na krosi ya Maftah.

Timu hizo ziliendelea kuoneshana uwezo kwa kushambuliana kwa zamu na dakika ya 19, Mike Mutyaba aliisawazishia timu yake bao kwa shuti la umbali wa mita 25, lililotinga moja kwa moja wavuni na kumwacha kipa Juma Kaseja, akilifuata bila mafanikio.

Kusawazishwa kwa bao hilo, kuliifanya Simba icheze kwa kasi,  huku ikilishambulia lango la Bunamwaya, na dakika ya 23, nusura Mohamed Banka aifungie Simba bao la pili, baada ya shuti lake kugonga mwamba na kurudi ndani, lakini mabeki waliondosha hatari.

Kipindi cha pili kilianza kwa kupooza huku kila moja ikitafakari la kufanya,  lakini Simba dakika ya 67, ilifanya shambulizi la kushtukiza baada ya Nassor Said 'Cholo' aliyeingia badala ya Derick Walulya aliyeomba kutoka,  kupiga krosi iliyotua kichwani kwa Shija Mkina aliyeingia badala ya Mussa Hassan 'Mgosi', lakini mpira ulitoka nje.

Bunamwaya ilionekana kama kuchoka kutokana na sehemu ya kiungo ikuruhusu Simba kutawala na kuliandana lango lao, ambapo dakika ya 75, Ulimboka Mwakingwe alikosa bao la wazi kwa kubaki na kipa Hamza Muwonge, baada ya shuti lake kutua miguuni kwa kipa huyo.

Maelfu ya mashabiki waliokuwepo uwanjani hapo wakijua mchezo huo utakwisha kwa changamoto ya mikwaju ya penalti, ndipo Santo alipowainua vitini mashabiki hao kwa kufunga bao la ushindi lililowafanya mashabiki hao walipuke kwa shangwe.

Simba: Kaseja, Walulya/Cholo, Maftah, Juma Nyosso, Kelvin Yondan, Santo, Mgosi/Mkina, Patrick Mafisango, Boban, Banka na Mwakingwe.

Katika mchezo mwingine uliopigwa mapema saa nane, El Merreikh ilitinga hatua hiyo kwa mikwaju ya penalti 9-8, baada ya kumaliza dakika 90 zikifungana bao 1-1.

El Merreikh ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuliona lango na Ulinzi dakika ya 85, lililofungwa na  Jonas Sakwawa na lilisawazishwa dakika ya 88 na George Othiene kwa kichwa, baada ya kuunganisha mpira wa krosi wa Stephen Waruru.

Baada ya dakika 90 kumalizika kwa matokeo hayo, ndipo mwamuzi Loluseghed Michael kutoka Eritrea, aliamuru zipigwe penalti.

Katika mikwaju hiyo ya penalti, El Merreikh iliibuka na ushindi wa penalti 9-8 na kusonga mbele hatua ya nusu fainali.

No comments:

Post a Comment