Na Godfrey Ismaely, Dodoma
SERIKALI imesema kuwa ili kukomesha vitendo vya wizi wa kazi za wasanii imedhamiria kushirikiana na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na SADC kupambana na wizi
wa hatimiliki na kazi za wasanii wote.
Kauli hiyo ya serikali ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Nishati
na Madini, Adam Malima kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Esther Bulaya (CCM).
Alisema kutokana na changamoto zilizojitokeza katika mpango wa awali wa
kupambana na wizi wa kazi za wasanii, serikali katika kipindi cha miaka
mitano ijayo, imepanga kutekeleza utaratibu wa wasambazaji wote wa kazi za
wasanii kubandika stika ya usalama ijulikanayo kama Hakigram kwenye kila
nakala ya kazi itakayosambazwa, ili kuhakikisha kazi za wasanii haziibwi.
“Katika utaratibu huu, kila msambazaji ataingia mkataba na msanii
kusambaza idadi fulani ya nakala na kupewa stika za Hakigram ambazo zitabandikwa kila nakala.
“Kwa maana hiyo, nakala za kazi ambazo hazina stika zitatambuliwa kama
nakala bandia na kuondolewa katika soko. Hakigram zitatolewa na Chama cha
Hakimiliki cha Tanzania (COSOTA) na tayari muundo wa Hakigram hizo umetayarishwa,” alisema.
Alisema wizi wa kazi za wasanii ni kosa la jinai na yoyote anayejihusisha na wizi huo, atachukuliwa hatua za sheria.
Naibu Waziri huyo alisema serikali ilifanya tathmini na kubaini ukubwa wa
soko la kazi za wasanii kupitia soko la kanda za sauti na CD ulifikia
nakala milioni 20 kwa mwaka.
Alisema hali hiyo inatokana na ukweli kwamba, kanda zinazozalishwa nchini
zinauzwa katika nchi jirani za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Malawi, Rwanda na Zambia, na
kuongeza kuwa, mauzo hayo hayakuwanufaisha wasanii wa Tanzania wenye
hakimiliki na serikali kwa ujumla.
“Utafiti huo pia umebaini kwamba, nakala nyingi za kanda kati ya hizo zilikuwa
zinauzwa kinyemela na ni bandia. Kwa wakati huo, bei ya mikanda ya sauti
ilikuwa sh. 1,000, mkanda wa video sh. 1,500 na CD sh. 3,000, biashara hiyo ingeweza kuingiza sh. bilioni 20 kwa mwaka,” alisema.
Malima alikuwa akijibu swali la Bulaya, aliyehoji serikali ina mkakati
gani mpya katika kipindi cha miaka mitano ijayo kupambana na wizi wa kazi za
wasanii, hasa baada ya mikakati ya awali kushindwa na kuhoji iwapo serikali
imefanya tathmini ili kubaini ni kiasi gani cha mapato kinapotea kutokana na
kazi za wasanii kuuzwa kinyemela.
No comments:
Post a Comment