28 July 2011

Yanga yajichimbia Jangwani

*Yadai inaiga kambi za Ulaya

Na Zahoro Mlanzi

KLABU ya Yanga inatarajia kuweka kambi ya wiki moja nje ya Makao Mkuu ya timu hiyo Mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam, kwa ajili ya
kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii na Ligi Kuu Bara.

Mbali na hilo, klabu hiyo leo inatarajia kutoa ufafanuzi juu ya suala la mchezaji wao mpya wa timu ya Taifa ya Uganda 'The Cranes', Hamis Kiiza kutokana na kushindwa kuwasili kwa wakati.

Akizungumza makao makuu ya klabu hiyo jana, mara baada ya kumalizika kwa mazoezi ya timu hiyo, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu, alisema kwa sasa wanafanya maandalizi ya ligi kuu kwa makini zaidi na ndio maana mpaka sasa wapo klabuni kwao wakiendelea na mazoezi.

"Wewe umeona wapi timu inakaa kambini kwa wiki moja, hebu angalia wenzetu Manchester United, Arsenal na Barcelona,  ulishasikia wanakaa kambini mwezi mzima, sisi tunataka kubadilika na kuachana na dhana zisizo za msingi," alisema Sendeu na kuongeza;

"Tutaendelea kujifua hapa hapa klabuni, lakini wiki moja ya mwisho, kabla ya mchezo wetu dhidi ya Simba wa Ngao ya Jamii, tutakwenda nje ili kujiweka sawa na mchezo huo," alisema.

Alisema kwa kuwa timu zetu hazina kipato cha kutosha, na kama wangekuwa nacho, wangefanya ziara ya kimichezo ili kujiandaa na msimu mpya wa ligi kuu.

Akizungumzia suala la Kiiza, Sendeu alisema mchezaji huyo wanafanya naye mawasiliano (lakini hakuweka wazi nini kinachoendelea), na kwamba jana jioni walitarajia kuzungumza naye tena na leo watalitolea ufafanuzi.

"Unajua si vizuri kutoa taarifa nusu nusu, leo (jana) nikizungumza hivi na kesho (leo) nikasema hivi, sidhani kama wana-Yanga watanielewa, hivyo naomba muwe wavumilivu kila, kitu kitakuwa wazi kesho," alisema Sendeu.

No comments:

Post a Comment