22 July 2011

Mbowe ataka kikosi kazi kutafuta umeme

Na Gladness Mboma, Dodoma

MBUNGE wa Hai, Bw. Freeman Mbowe ameendelea kuing’ang’ania serikali kuunda kikosi kazi kwa ajili ya kushughulikia tatizo la umeme nchini.Akiuliza swali la papo hapo kwa
Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, Bw. Mbowe alisema kutokana na serikali kushindwa kulimaliza tatizo hilo tangu mwaka 2008, hivi sasa ni wakati muafaka kwa serikali kuunda kikisi hicho, ili kulinusuru taifa na tatizo hilo.

Alisema udhaifu huo pia umeonekana katika uandaaji wa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, hali iliyosababisha upitishwaji wake kuahirishwa hadi Agosti 13, mwaka huu.

“Kitendo cha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kushindwa kupitishwa na kuahirishwa ni kielelezo tosha serikali imeshindwa na nidhaifu, ili kuliepusha taifa na tatizo hili huoni kwamba ni wakati muafaka wa kukubali kuunda kukosi kazi cha taifa ili kushughulikia tatizo hilo?” alihoji.

Akijibu swali hilo, Bw. Pinda alisema hawezi kuupuuza ushauri huo, lakini akasema serikali imejipanga katika kutatua tatizo hilo kwa muda mfupi na kwa hatua za haraka.

“Hili jambo la umeme nimelizungumzia mara kwa mara lakini ngoja nirudie kukujibu. Serikali itanunua mtambo wa megawati 100 katika kutatua tatizo kwa muda mfupi, lakini ni lazima tuwe na mfumo wa kuwa na umeme wa uhakika.

"Tuliahirisha jambo hili ili serikali iweze kujipanga, tukirudi tutakuja na mpango wa kuwa na umeme wa uhakika,” alisema.

Bw. Pinda alimwomba Bw. Mbowe kuipa serikali nafasi na kama itashindwa kutekeleza hilo, ishikwe kwa uongo.

“Mimi nashughulika na umeme wa dharura, kwa mpango wa muda mrefu hatutashindwa kushughulikia tatizo hili. Kama utaendelea kuniuliza swali hili, nami majibu yangu yatakuwa ni hayo hayo,” alisema.

2 comments:

  1. Kila siku serikali inaendelea kujipanga, kujipanga huku kuna maana gani jamani,
    Hapa kinachotakiwa ni kuunda timu ya wataalam kutoka hapa hapa nchini na kuwawezesha pesa nyingi kuliko hata iliyokuwa inataka kuhongwa iliwaweze kuja na proposal nzuri. Wanasiasa wasihusishwe na timu hii kwani hawana cha kufanya hapa ila wao wasubiri kujigamba baaada ya suluhishi kupatikana.

    Pia suala kama hili si mpaka wapinzani waseme jamani. Ni letu sisi sote na pia nawapeni hongera sana juu ya hili.

    Otherwise mie nawatakieni kila la heri

    ReplyDelete
  2. Mh.Mbowe point yake ni ya mhm sana. Sijui serikali inashindwa nni, jitihada zao mara zote wanakuja kuumbuana ufisadi! Msikilize Mbowe!

    ReplyDelete