Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MBUNGE wa Arusha Mjini, Bw. Godbless Lema (CHADEMA) amemtuhumu Mbunge wa Viti Maalumu, Bi. Mary Chatanda (CCM) kuwa ndiye chanzo cha mauaji
yaliyotokea mkoani Arusha Januari 5, mwaka huu ambapo watu watatu waliuawa.
Bw. Lema alitoa tuhuma hizo bungeni jana, wakati alipoomba mwongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge, Bw. Sylivester Mabumba juu ya taarifa zilizotewa na Bi. Chatanda wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Wakati akichangia hotuba hiyo, Bi. Chitanda alipongeza muafaka uliopatikana kati ya madiwani mkoani Arusha, ambao hata hivyo unapingwa na CHADEMA Makao Mkuu, wakidai kuwa mazungumzo hayo hayakuwahusisha.
Katika hilo, Bw. Lema alisema taarifa hizo si kweli na kwamba CHADEMA haikuwahi kufikia muafaka wowote.
Bw. Lema alisema chanzo cha mauaji ya Arusha ni Bi. Chatanda, kwani wakati anazungumza aliwashukuru wanawake wa Tanga kwa kumchangua.
“Arusha ni jimboni kwangu, namwambia hakuna muafaka kama anautafuta aendelee kuomba,” alisema.
Kutokana na taarifa hiyo, Bi. Chatanda naye aliomba mwongozo wa Mwenyekiti kwa kueleza kuwa Bw. Lema ametumia kauli za kuudhi kwa kusema yeye ndio chanzo mauaji hayo.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu mbunge Lema amenituhumu kuwa chanzo cha mauaji Arusha, hiyo ni kauli ya kudhalilisha, kuudhi na kunisingizia. Ningekuwa nimefanya mauaji ningeshtakiwa. Naomba mwongozo wako mwenyekiti,” alisema.
Akijibu hoja hiyo, Mwenyekiti Bw. Mabumba alisema suala hilo lipo mahakamani na mahakama ndiyo itakayotoa uamuzi.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Bi. Faida Bakari alisema kuwa mbunge wa Ziwani (CUF), Bw. Ahmed Juma Ngwali amekuwa akiwadharau wabunge wa Viti Maalumu na kumtahadharisha kuwa mwaka 2015 hatapata ubunge.
“Namwambia mimi nilikuwa mbunge wa jimbo na sasa ni wa Viti Maalumu, Bw. Ngwali anatudharau wabunge wa Viti Maalumu namwambia ujiti na macho, mwaka 2015 hatapata ubunge,” alisema.
Hali hiyo ilisababisha mbunge wa Ole, (CUF), Bw. Rajab Mbarouk Mohammed kuomba kutoa taarifa kwa bunge na kusema: “Mheshimiwa Faida si kwamba mtachukua jimbo la Ziwani, wewe na chama chako hamna uwezo wa kuchukua jimbo lolote Pemba”.
Akichangia mjadala huo, aliomba kuwapo na sheria ya kuwabana wanaume wanaotelekeza familia zao, kwani kitendo hicho kinachangia kuwapo kwa watoto wa mitaani.
Kwa upande wake, Bi. Bakari alikemea suala la watu wa jinsia moja kuwa na uhusiano wa kimapenzi, kwani suala hilo linakemewa hata katika kitabu vya dini.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba itungwe sheria ili kuwadhibiti watu wenye tabia hii, kwani ni vibaya hata katika maandiko ya dini zetu,” alisema.
No comments:
Post a Comment