22 July 2011

Msidanganywe na kampuni za mikopo-Pinda

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WATANZANIA wameshauri kutokuwa wepesi kudanganywa na kampuni zinazokuja na kudai kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwani nyingi niza kitapeli.Kauli hiyo
ilitolewa bungeni jana na Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda na kusema kampuni hizo zinapoingia nchini huwalenga watumishi wa umma, hasa walimu.

“Chonde chonde walimu msiwe wahanga wa suala hili, kwani yapo makampuni yanayokuja kwa njia ya ujanja na kudai kutoa mikopo yenye masharti nafuu, yakiwamo kampuni ya Bayport na Deci” alisema.

Alisema yanapojitokeza makampuni kama hayo, tatizo wananchi wanajiingiza kichwakichwa bila kuishirikisha serikali, hivyo inapobainika hali hiyo si sahihi kubebesha mzigo serikali.

Bw. Pinda alikuwa akijibu swali la mbunge wa Muhambwe (NCCR MAGEUZI), Bw. Felix Mkosamali aliyehoji kama serikali ipo tayari kuyafungia makampuni yanayowatapeli wananchi kama kampuni ya Bayport na Deci.

Wakati huo huo, mbunge wa Sumve (CCM), Bw. Richard Ndassa alihoji serikali inatoa tamko gani kutokana na kushuka kwa bei ya pamba.

Akijibu swali hilo, Bw. Pinda alisema bei ya pamba katika soko la dunia imeshuka kutoka sh 1,100 hadi sh 800, hivyo kushauri wakulima kuelimishwa kuhusu suala hilo na kuongeza kuwa wanunuzi wa pamba waruhusiwe kununua kwa bei wanayoitaka.

2 comments:

  1. Pinda kama kiongozi wa serikali kwanini mnayaruhusu hayo makampuni ya kutoka nje yenye masharti nafuu kuja kuwekeza hapa nchini wakati mnajua kabisa mwisho wake ni watu kutapeliwa alafu eti serikali ndio ingilie kati.Unajuwa wawekezaji wameshajua viongozi wetu ni walafi na wanapenda 10% na ndio maana wanakuja kuwekeza kiubabaishaji Tanzania kwa sababu wanajua kila kitu kinavyo kwenda.Kiongozi akishapokea mshiko wake ndio basi tena yatakayofuatia baadae hayo ni matatizo ya wananchi yeye hajali kitu kwani anajua wapo rafiki zake katika uongozi wa juu watakaompigia kifua.halafu inafuatia kauli ya huu mjadala umeshafungwa hivyo hauitajiki tena kujadiliwa,Waziri mkuu amesema.

    ReplyDelete
  2. Nasikitishwa na majibu hafifu yanayotolewa na hawa viongozi wetu. Mimi ni mhanga wa Bayport. Hawa watu wana utapeli wa hali ya juu. Wana pia mbinu nyingi za kuchukua fedha za watu. Kwangu nimejikuta nimekatwa mshahara wangu na katika kufuatilia nikagundua kuwa Bayport ndio wamekata mshahara huo. Sijawahi kuwasiliana nao kwa swala la mkopo. Nimewafuata na salary slip yangu wanajibu mbovu. Hawajanipa hio hela na mshahara wamekata. Sijawahi kujaza fomu zao hata siku moja. Naomba katika haya ya makampuni ya kukopesha serikali iingilie kati. Au wanaogopa kwa kuwa baadhi ya vigogo wana hisa katika kampuni hizo?

    ReplyDelete