Na Zahoro Mlanzi
KOCHA Mkuu wa timu ya Bunamwaya ya Uganda, Golola Edward amesema ushindi wa jioni wa Yanga umesababishwa na uzembe wa kipa wake, Hamza Muwonge kwa
kutokuwa makini golini.
Aliyasema hayo mara baada ya kumalizika kwa mchezo kati ya timu yake na Yanga, uliopigwa juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 na kutinga robo fainali ya mashindano ya Kagame Castle Cup.
Edward alisema hakutarajia kama wangefungwa dakika hizo, kwani matumaini yake yalikuwa ni kuondoka na pointi moja hasa kutokana na Yanga kuonekana kuwa na uzoefu kuliko wao.
"Yanga ni timu bora Tanzania, hilo nalijua lakini tuliweza kukabiliana nayo mpaka dakika za mwisho na kama si uzembe wa kipa, sina shaka kila timu ingeondoka na pointi moja," alisema Edward.
Alisema ni mara yake ya kwanza kushiriki mashindano hayo na timu nyingi zina uzoefu kasoro timu yake lakini, ana matumaini ya kuingia robo fainali kama 'best looser' kutokana na matokeo anavyoyaona Kundi C lililopo Morogoro.
Wakati huohuo, Kocha Mkuu wa Yanga, Sam Timbe alisema licha ya timu hiyo kutokuwa na uzoefu wa michuano ya kimataifa lakini wametoa ushindani wa nguvu.
Alisema mchezo huo ulikuwa mgumu sana kutokana na kila timu kuhitaji pointi tatu ili ijihakikishie nafasi ya kucheza robo fainali ya mashindano hayo na pia alikiri beki wake Shadrack Nsajigwa, alimtoa kutokana na kuzidiwa na presha langoni mwake.
No comments:
Post a Comment