12 July 2011

CUF wamvaa Sitta

*Wadai amewakebehi Wazanzibari kuhusu muungano
*Watakiwa kusimama bila ya woga kutetea nchi yao


Na Mwajuma Juma, Zanzibar

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimemvaa Waziri wa Afrika Mashariki, Bw. Samuel Sitta kikimtaka aache kuwakebehi Wazanzibari kwa kauli alizotoa
bungeni kuhusiana na muungano.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Bw. Ismail Jussa Ladhu amesema wakati umefika kwa Wazanzibari kusimama kidete na bila ya woga kuitetea Zanzibar katika masuala mbalimbali ya Muungano.

Wiki iliyopita Bw. Sitta akijibu hoja mbalimbali za wabunge wakati akichangia bajti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, alipinga kuanzishwa kwa serikali tatu, akisema itakuwa ndio kuua muungano, kwa kuwa itahatarisha ustawi wa Zanzibar.

"Kuleta serikali tatu ni kumleta mbia wa kushindana na Zanzibar na hapo Tanganyika haitakubali, kwani wote watalazimika kuichangia serikali ya tatu na hapo haitakuwa na meno ... kwa sababu ya Muungano, Zanzibar inauziwa umeme kwa bei ndogo na sasa tunaidai sh bilioni 50, lakini tumekaa kimya.

"Kwa akili nyepesi kutaka serikali tatu ni kuua Muungano, kama Muungano hautakiwi semeni kistaarabu tuwe na maelewano ... tuache kusema Karume (Abeid) alikuwa mbumbumbu wakati alifanya mazuri mengi kama kujenga nyumba za Michenzani," alisema.

Pia waziri huyo, alisema wakati wa mjadala wa Muungano baina ya waasisi wake, Mzee Abeid Aman Karume alikuwa anataka uwe wa serikali moja na yeye awe Makamu wa Rais, lakini Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alisema ikiwa hivyo Zanzibar itamezwa, hivyo akashauri ziwe serikali mbili, kama ilivyo sasa.

Kutokana na kauli hiyo, Bw. Jusa aliyeonekana kukerwa na kauli hizo za Waziri Sitta, alisema wakati huu Wazanzibari wote wanahitaji kupata haki sawa juu ya mambo yanayohusu Muungano. Alimtaka na kuwabeza Wazanzibari wakati wanaposimama kudai haki zao.

Bw. Jussa alitoa kauli hiyo jana wakati akiwahutubia wananchi na wanachama wa chama hicho Jimbo la Bububu, Wilaya ya Magharibi Unguja.

Alisema, Bw. Sita amekuwa akitoa matamshi mabaya juu ya lengo na adhima ya muungano, jambo ambalo halileti taaswira nzuri.

"Kwenye muungano huu kila nchi inapaswa kupata haki sawa na mwenzake na mambo ambayo hayamo katika muungano yanapaswa yasiingiliwe,” alisema.

Alisema kuwa Marehemu Karume na Mwalimu Nyerere walitaka kuwepo na muungano wenye maslahi bora kwa pande zote mbili.

Lakini kinyume na hilo, Bw. Sitta amekuwa akibeza muungano kwa kusema mambo ambayo hayamo katika makubaliano, huku akifanya Wazanzibari kama watu wasioelewa adhima ya muungano huo.

“Huu si wakati tena wa kutudanganya, Wazanzibari wa leo tumesoma hatudanganyiki,” alisema Bw. Jussa na kupigiwa makofi na wananchi waliokuwepo.

Alisema kuwa katika Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Wazanzibari wamependekeza mambo kadhaa ambayo kutoingizwa kwake kutasababisha mswada huo kutopita.

"Kama alivyosema Mzee Karume Muungano ni sawa na koti, hivyo likitubana tutalivua," alisema.

Aidha aliwaambia wananchi hao kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua ahadi kuwa itasimamia kidete kuhakikisha maslahi ya Zanzibar yanalindwa.

Akijibu malalamiko ya wabunge waliochangia kuwa suala la mafuta kuwekwa kwenye Muungano baada ya kuwa na dalili ya kupatikana Zanzibar, Bw. Sitta alisema serikali ililazimika kuliingiza kwenye Muungano, baada ya kubainika kuna uwezekano wa kupatikana mafuta baharini kwenye mpaka kati ya Tanga na Pemba.

"Hapo huwezi kujua mafuta yatapatikana wapi, hivyo kuepuka ugomvi na yasitokee kama ya Iraki na Kuwait, tukaona tuliingize kwenye Muungano," alifafanua.

Kuhusu mambo ya Muungano kuongezwa kutoka 11 hadi 22, alisema yaliongezwa kulingana na matukio kama kulipovunjika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na hayakuongezwa kiholela, bali Bunge lilipitisha kwa kupiga kura. Alitaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni Posta na Simu; Hali ya Hewa na Ofisi ya Takwimu.

Hata hivyo, alisema, suala la elimu ya juu liliingizwa baada ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuiomba Serikali ya Muungano kwa barua ambayo hadi leo ipo imehifadhiwa.

Akizungumzia ushiriki wa Zanzibar kwenye masuala ya Afrika Mashariki, alisema "ushiriki wake ni wa moja kwa moja, kabla ya kwenda huwa wataalamu wa pande zote wanakutana na baadaye mawaziri tunakwenda kwenye majadiliano."

Alitaja miongoni mwa miradi ya maendeleo ya Zanzibar iliyotokana na ufadhili kupitia EAC, kuwa ni pamoja na ujenzi wa uwanja wa ndege wa Karume kisiwani Pemba; bandari ya Marhubi; ujenzi wa chelezo ambapo mtu ataweza kusafiri na gari hadi Mombasa au Dar es Salaam.

11 comments:

  1. Huyu bwana anasema wazanzibar wamesoma sasa hawawezi kudanganywa lakini cha ajabu hajajibu hoja ya Sitta. Kwa ufupi wanatakiwa waseme kama hawautaki Muungano waseme hawautaki basi! Ninadhani ndoa ya kubembelezana huwa haidumu naamini kwa mda mrefu wazanzibar wamebembelezwa sana juu ya Muungano lakini hawautaki tutabembeleza mpaka lini jamani? Muungano hauna faida yeyote kwa wabara ila ni kwa faida yao. Na mara nyingi wanachong'an'gania ni madaraka ya kuongoza. Na hao yanasemwa na viongozi walafi wa madaraka. Mara wanataka mabalozi mara wawe wakubwa wa jeshi. Bila kuangalia elimu na udhoefu mladi tu wapate vyeo. Wakati huo huo hawazungumzii wazanzibar na hasa wapemba wanaofanya biashara na wanamifugo yao mpaka Shinyanga. Naamini hawa watu wakawaida wapemba wakiulizwa juu ya muungano wataunga mkono kwani ukifa waende wapi na mifugo yao. Zanzibar ni ndogo haiwezi kuhimili wingi wa watu lakini kwa sababu ya muungano wanafaidika. Kisa baadhi ya wanasiasa wanataka vyeo! Jamani hata Zanzibar ikijitenga haiwezi kuwa na balozi kiasi kwamba kila mwanasiasa anaweza kuwa balozi. Nchi nyingi zinapunguzi balozi zao wao wataongeza balozi za nini ili tu eti wapewe vyeo bila kuangalia kama uchumi wao utaruhusu au la! Waseme kama hawautaki Muungano basi ufe kila mmoja ajue ustarabu wake. Wakati wa kuwabembeleza wazanzibar umepita sasa. Mara watakekuwa kwenye Jeshi. Jeshini watu wanaajiliwa kutokana na sifa zao. Hata akiwa mzanzibar akiwa na ujuzi anaajiliwa na anaweza kuwa mtu mkubwa tu mladi awe na ujuzi unaotakiwa. Kwenye mambo ya taaluma hakuna kupendeleana ama sivyo tutakuwa na jeshi la watu mbumbu ambao hawawezi kutumia zana za kisasa ambazo zinataka mtu awe amesoma sana. Mtu asiyetegemea elimu ya madrasa! Kwani kule haendi kusomesha kurani. Someni mpate degree za kweli ili muweze kupata kazi sio tu za jeshi hata za mashirika ya kimataifa. Ninyi msitafute visingizio semeni tu muungano hapana muwone kama mtaungwa mkono na wazanzibar wa kawaida. Wao wanachotaka ni kuendesha maisha yao bila woga wa vibano vya kuwa na nchi ndogo. Mambo ya siasa kwao hayana maana yeyote! Mheshimiwa speaker amewaambia kama hamtaki muungano mseme wakati wa mapendekezo ya katiba mpya hapo ndo mtajua kama mnaweza kuungwa mkono na wazanzibar wakawaida. Wao wanafanya biashara zao bara bila matatizo yeyote baadhi yao wanajishughulisha na kilimo bila shida yeyote. Sasa leo uwaambie hutaki muungano nakwambia hao hawatakuelewa ndugu yangu wewe unayetaka kuwa balozi na mkuu wa majeshi!

    ReplyDelete
  2. Hakuna haja wala sababu ya kuendelea kutoleana maneno, ni kura tu ya maoni, ipigwe na wananchi wote kama South Sudan! then tutajua mbichi na mbivu! na tusijuane baada ya hapo, maana mpaka wetu hauna utata

    ReplyDelete
  3. wapeni nchi yao musijifanye waizrail nyinyi watanganyika

    ReplyDelete
  4. hamutaki kuweka maoni ya wanzanzibar mbona, munachanguwa

    ReplyDelete
  5. MH Jumbe kasema muungano basi, mukamkamata

    ReplyDelete
  6. munataka wanzibar waseme mulete majeshi mutangaze hali ya hatari visiwani muvichukuwe visiwa kwa nguvu kupitia majeshi

    ReplyDelete
  7. Kisiwe kisingizio cha kusema wapemba wanaofanya biashara Tanganyika watakwenda wapi Ukivunjika Muungano feki? Tujiulize bila ya kuumiza Vichwa .Wasomali,Wahindi,Wakenya, Wayemeni nk. wote hao si Wanafanya biashara Tanganyika Je wote hao Wameungana na Tanganyika.Wapo na wanaendelea kuwepo na wanafuata taratibu za nchi husika na wapemba watafuata utaratibu hizozo kama wazozifuata Wasomali n.k

    ReplyDelete
  8. what the hell this mdudu muungsno is! halafgu ni kwa nini munawauzia umeme kwa bei ndogo?ili iweje?

    ReplyDelete
  9. Mtoa maoni wa kwanza anadhani kuwa alichoandika kuwa ni maneno mazima....sasa kwa wazanzibar kuwa na mifugo au maduka haizui watu kusema na kutetea maslahi ya umma na nchi kwa ujumla.....sisi quran inatutosha sana...hayo maphd chukueni nyinyi kwani kila mkisoma zaidi ndio wazungu magoigoi wanapozidi kuwaibia rasilimali zenu.....elimu inawasaidia watu wote duniani ispokuwa watanganyika....soo saad!!!

    ReplyDelete
  10. Nimechoka na kauli za wazanzibar kuwa hawaoni faida za muungano. Mimi kama mimi napendekeza kuwe na serikali moja kama haiwezekani muungano ufe, tusibembelezane hapa tumechoka na watu wanaopiga kelele za muungano. muungano ufe jamani tumechoka na kauli zao.

    ReplyDelete
  11. AMA TUWE NA SERIKALI TATU (Shirikisho) au SERIKALI MOJA (Muungano ).MUUNGANO WA SASA NI KERO KWA PANDE ZOTE MBILI. NADHANI UPATIKANAJI WA MAFUTA UTATULETEA MUUNGANO AU SHIRIKISHO. ONGEZENI BIDII WAZANZIBAR!!

    ReplyDelete