20 June 2011

Wamiliki mbwa waliokula mahindi kudaiwa fidia

Na Mashaka Mhando, Korogwe

SIKU mbili baada ya kuripotiwa habari za mbwa wanane kuvamia mashamba ya wakulima na kula mahindi machanga, wakulima walioathirika na tukio hilo
wamembana mmiliki wa wanyama hao wakitaka walipwe fidia.

Hii ni mara ya pili tukio la mbwa kuvamia mashamba na kula mahindi machanga, mara ya kwanza ikiwa Agosti 2008 ilipotokea katika Kata ya Kitembe, wilayani Rorya mkoani Mara waliharibu mazao hayo na kusababisha wasiwasi mkubwa wa baa la njaa kwa wakazi wa eneo hilo.

Safari hii mkasa huo umewakumba wakulima Mji wa Old Korogwe, ambapo sasa wakulima wanataka walipwe fidia na wamiliki wa mbwa hao.

Kama ilivyokuwa tukio la Mara, uharibifu uliofanywa na mbwa hao wa Korogwe pia unatishia kutokea kwa njaa endapo hali hiyo ikiendelea.

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Old Korogwe, Bw. Kassim Lupatu, alimtaja kwa jina moja, mmoja wa wakulima ambaye mazao yake yameliwa na mbwa hao kuwa ni Bw. Mussa.

Alisema katika shamba la Bw. Mussa mbwa hao walikula kiasi cha mashina 936 ya mahindi. Mashamba mengine yaliyoharibiwa na mbwa hao, kuwa ni ya Mama Mziray na lingine la Bw. Daud Kayoka.

Alisema wakulima hao wana mashamba yao eneo la Habitat Mji Mpya, Mjini Korogwe.

Alisema baada ya kuwaona mbwa hao wakifanya uharibifu huo, waliamua kuwasaka ili kuwaua, lakini  kabla ya kufikia uamuzi huo waliomba viongozi wafanye utaratibu ili wamiliki wa mbwa hao waweze kuwalipa fidia.

Mjumbe huyo aliwataja kwa majina wamiliki wa mbwa hao (majina yanahifadhiwa).

Akielezea ukweli wa mbwa hao kula mahindi hayo shambani, Bw. Lupatu alisema wakulima hao baada ya kuona tukio hilo walitoa taarifa kwa uongozi wa serikali ya mtaa ambao haukuamini.

Alisema viongozi hao walipopelekwa mashambani kukagua uharibifu huo, waliwakuta mbwa hao wakila mahindi hayo huku wengine wakiacha kinyesi ambacho kilionekana kuwa na mchanganyiko wa mahindi.

Kutokana na tukio hilo wakulima hao wametaka wamiliki wa mbwa hao wawalipe fidia hasa kwa kuzingatia kuwa wakulima hao walitumia mbegu za kisasa na mbolea.

Viongozi hao wa serikali ya mtaa, wamewaandikia barua wakulima hao kufikisha malalamiko yao kwenye uogozi wa baraza la kata kwa hatua zaidi.

No comments:

Post a Comment