23 June 2011

Tumefuata taratibu kugawa vitalu-Wizara

Na Rabia Bakari

WIZARA ya Maliasili na Utalii imetoa ufafanuzi kuhusu tuhuma za kuwabeba raia wa kigeni katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji, na kudai kuwa imegawa kwa
kuzingatia taratibu na kanuni za kisheria ambazo zilikuwa wazi kwa kila mwananchi.

Msemaji wa Wizara hiyo, Bw. George Matiku alisema kuwa kuna baadhi ya vyombo vya habari vinapotosha umma kwa madai kuwa kuna mikakati ya kuwabeba wazungu katika suala la uagwaji wa vitalu.

"Tunatoa ufafanuzi kuhusu kuongeza muda wa kukamilisha mchakato wa kuwateua waombaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii katika kipindi cha mwaka 2013 hadi 2018.

"Hii imetokana na uamuzi wa wizara wa kutoa tangazo jingine kupitia vyombo vya habari linalowataka wadau kuleta maombi kwa vitalu ambavyo havikupata waombaji au waombaji wake hawakuwa na sifa za kumilikishwa vitalu," alisema Bw. Matiku katika taarifa yake.

Aidha aliongeza kuwa taarifa za kutaka kuwabeba wazungu katika suala hilo si la kweli, huku akisisitiza ubaguzi siyo sehemu ya sera za wizara na ni kinyume na katiba ya nchi.

"Vitalu vinagawiwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo bila kubagua mtu kutokana na rangi au utaifa wake," aliongeza kudai.

Alisema kuwa baada ya kanuni za uwindaji wa kitalii kukamilika, Februari 10, mwaka huu wizara ilitoa tangazo kupitia vyombo vya habari lililowataka wadau wa tasnia ya uwindaji wa kitalii kupeleka maombi yao ya kupatiwa vitalu vya uwindaji kwa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori.

Aliongeza kuwa matangazo hayo yaliambatana na sifa pamoja na vitu anavyotakiwa kuna navyo muombaji ambapo baada ya hapo maombi yalifanyiwa uchambuzi na kamati ya ushauri wa ugawaji wa vitalu ambayo ilitoa taarifa yake yenye mapendekezo kwa waziri ambapo moja kati ya mapendekezo yaliyotolewa ni pamoja na kuongeza muda kwa ajili ya kujiridhisha kuhusu masuala mbalimbali ambayo wizara haina iwezo nayo.

"Masuala hayo ni pamoja na uhalali wa dhamana za benki, taarifa za waombaji kuhusu ulipaji wa kodi, uraia wa baadhi ya wenye kampuni na wanahisa wake pamoja na uhalali wa kampuni zilizoomba vitalu.

"Ni dhahiri kuwa wizara haina uwezo wa kufanya uhakiki wa taarifa hizo, hivyo ulihitajika muda wa kutosha kuwezesha vyombo vinavyohusika kufanya uhakiki huo.

"Kwa kuwa kulikuwa na vitalu ambavyo havikupata waombaji au waombaji wake hawakuwa na sifa stahili, kamati ilishauri vitalu hivyo vitangazwe ili uhakiki wa baadhi ya waombaji ufanyike sambamba na uhakiki wa waombaji wapya ili kuokoa muda na fedha," aliongeza Bw. Matiku.

No comments:

Post a Comment