Na Peter Mwenda
CHUO Kikuu cha Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma(SJMC) kimetakiwa kutoa mafunzo ya uandishi wa habari yatakayowawezesha wahitimu kukabiliana na
changamoto zinazoikabili taaluma hiyo.
Akizindua mafunzo ya Shahada ya Uzamili na Mawasiliano ya Umma ya SJMC, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala, alisema wakati Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinaadhimisha miaka 50, mafunzo mbalimbali yanayotolewa yanatakiwa yaoneshe matunda katika jamii.
Profesa Mukandala alisema inafurahisha kuona SJMC kuwa na vyombo vyake vya habari ili kutoa mfano wa taaluma ya habari inavyotakiwa.
Alisema Shahada ya Uzamili itakayoanza kutolewa itasaidia kukidhi kiu ya Watanzania kupata wataalamu wa fani hiyo wataosaidia Tanzania kupitia taaluma ya habari ambayo inakuwa kwa kasi.
Awali Mkuu wa Chuo cha SJMC,Dkt. Bernadeta Killian, alisema chuo hicho kilianza mwaka 1975 kikiwa kinamilikiwa na Serikali ya kikijulikana kama Chuo cha Uandishi wa Habari Tanzania (TSJ) kikitoa vyeti na stashahada ya uandishi wa habari ambapo kila mwaka walihitimu wanafunzi 30.
Dkt. Bernadeta alisema wahitimu wa TSJ wakati huo walikuwa wakiajiriwa na vyombo vya habari vya Serikali na Idara ya Habari (Maelezo), lakini sasa vyombo vya habari ni vingi vikiwemo vya binafsi na Serikali.
Alisema mwaka 2003 TSJ kiliunganishwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kuwa (SJMC) kikitoa mafunzo ya masomo ya uandishi wa habari kutoka ngazi ya cheti mpaka Shahada ya Uzamili iliyozinduliwa jana.
Alisema uhuru wa vyombo vya habari umewafanya watanzania wapate habari mbalimbali kutoka vyombo vya Serikali na binafsi vinavyofikia magazeti na majarida 63, vituo 72 vya redio na televisheni 39 ambavyo waaandishi wake wametokana na chuo hicho.
Dkt. Bernadetha alisema ili kufikia malengo ya chuo hicho kuwa bora ya elimu ya habari na mawasiliano ya umma kimepanga kutoa wataalamu walibobea katika fani hiyo,kufanya utafiti wa taaluma hiyo nchini na kushirikiana na vyuo vingine vya Tanzania na kimataifa.
Alisema SJMC pia kitaboresha taaluma ya habari nchini na kutoa mafunzo ya kisasa ya uandishi wa habari na mawasiliano ya umma kwa kiwango cha juu.
No comments:
Post a Comment