09 June 2011

Serikali kupitia upya VAT

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2011/2012 inakusudia kufanya mapitio mapya ya utaratibu wa misamaha kwenye Kodi ya Ongezeko la
Thamani (VAT).

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Fedha, Bw. Mustapha Mkulo, wakati akisoma Bajeti ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2011/2012.

Maeneo aliyotaja kuwa kodi ya VAT inakududiwa kufanyiwa marekebisho ni kwenye mashudu ambayo ni chakula cha mifugo, vifaa vya kutotolea vifaranga na vifungashio.

Alisema kuwa maeneo mengine ambayo yanakusudiwa kufanyiwa marekebisho kwa kuondoa kodi ni kwenye vifaa vya kufyekea, mashine za kupandia mpunga, mbegu na trekta za mikono.

Alisema pia marekebisho hayo yatagusa nyuzi za kutengeneza nyavu za kuvulia samaki ili kuwapa nafuu wavuvi, vipuri vya kunyunyuzia dawa, kutifua udongo na kupandia.

Pia VAT itaondolewa kwenye kuuza na kupangisha nyumba za Shirika la Nyumba Tanzania (NHC). Aliongeza kuwa serikali itapunguza kodi kwenye posho wanazolipwa watumishi wake na kufuta kodi ya zuio kwa ndege zinazosafirisha minofu ya samaki.

Alisema hatua hiyo itaongeza usafirishaji wa samaki kwa wingi, ingawa katika eneo hilo serikali itapoteza mapato kwa uamuzi wake huo.

1 comment:

  1. Hivi lengo letu ni kusafirisha tu kwa wingi nje ya nchi hao samaki, dhahabu n.k. hata kama tunapoteza mamapato! Hizi ni takataka ambazo lazima ziondolewe?

    ReplyDelete