Na Reuben Kagaruki
SERIKALI imetangaza hatua madhubuti itakazozitumia kudhibiti matumizi ya fedha zake katika kipindi cha mwaka fedha 2011/2012, uamuzi ambao ulipokewa kwa
makofi kutoka kwa baadhi ya wabunge.
Uamuzi huo wa serikali ni wazi utawaathiri baadhi ya watumishi wa serikali waliokuwa wanategemea mianya hiyo kujiongezea kipato.
Hatua za kudhibiti matumizi ya fedha ilitangazwa mjini na Waziri wa Fedha na Uchumi, Bw. Mustapha Mkulo, wakati akisoma Bajeti ya Serikali Bungeni mjini Dodoma jana.
Alitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kusitisha manunuzi ya magari ya serikali yasiyo ya lazima. Kwa mujibu wa Bw. Mkulo kuanzia mwaka huu wa fedha magari ya serikali yatakuwa yakinunuliwa kwa kibali kutoka ofisi ya waziri mkuu.
Pia alitangaza hatua ya serikali kupunguza malipo ya posho mbalimbali yasiyo na tija na kupunguza matumizi ya mafuta kwa magari ya serikali.
Hatua nyingine zilizotangazwa na Bw. Mkulo bungeni ni za kudhibiti matumizi ya fedha za serikali, kupunguza safari za nje na ndani na kupunguza ukubwa wa misafara ya viongozi.
"Tutapunguza uendeshaji wa semina na warsha ikibidi zifanyike kwa kibali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu," alisema Bw. Mkulo huku akishangiliwa na baadhi ya wabunge.
Alitaja gharama zingine zitakazopunguzwa kuwa ni za uendeshaji maonesho pamoja na manunuzi ya thamani za maofisini kwa ajili ya ofisi za serikali.
No comments:
Post a Comment