09 June 2011

Mfumuko wa bei wakwamisha ukuaji wa uchumi

Na Pendo Mtibuche, Dodoma

WAZIRI wa Fedha na Uchumi, Bw. Mustafa Mkulo jana aliwasilisha  taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa na kubainisha vipaumbele ambavyo serikali imevipa umuhimu
katika bajeti ya mwaka 2011/2012.

Akisoma taarifa hiyo bungeni mjini Dodoma, na malengo ya uchumi katika kipindi cha muda wa kati ya mwaka 2011/2016, Waziri Mkulo alisema kuwa serikali imeamua kuchukua vipaumbele ambavyo vinatokana na changamoto zinazowakabili wananchi katika kukabiliana na hali ngumu ya maisha.

Alisema kuwa kwa sasa serikali inatambua umuhimu wa kujenga uchumi imara na wenye ushindani kwa kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa uhakika wa umeme ili kuwezesha shughuli za kiuchumi na maendeleo ya jamii kufanyika wakati wote.

Jambo jingine ambalo serikali italifanyia kazi ili kuimarisha uchumi ni kuongeza upatikanaji wa chakula kwa kuhimiza kilimo hasa cha umwagiliaji na kuimarisha hifadhi ya chakula ili kujikinga na tatizo la uhaba wa chakula nchini.

Alisema kuwa pamoja na kuimarisha miundombinu ya maji, reli, bandari, barabara na kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Saalam, pia serikali itaongeza fursa za ajira na kuwanufaisha wananchi wengi hasa vijana ambao ndio kundi kubwa katika soko la ajira.

Aidha wizara, idara na taasisi za serikali nazo zinaelekezwa kuzingatia suala la kuongeza ajira katika maeneo yao.

Kwa upande mwingine Bw. Mkulo alizungumzia hali ya kuwepo kwa mfumuko wa bei na kuwa hali hiyo ilisababishwa na kuongezeka kwa wastani wa bei za chakula, mafuta, umeme na gharama za uzalishaji na usafirishaji lakini akabainisha kuwa hatua zinachukuliwa ili kudhibiti ongezeko la bei za mafuta, chakula na kuongeza uzalishaji wa umeme.

Alisema pamoja na mfumuko wa bei kuendelea kuwa tarakimu moja umekua na mwelekeo wa kupanda hususani katika robo ya kwanza ya mwaka 2011 ambapo mfumko wa bei uliongezeka kutoka asilimia 5.6 kwa kipindi cha Desemba 2010 hadi kufikia asilimia 6.4 Januari mwaka huu ambao umeendelea kupanda hadi kufikia asilimia 8.6 Aprili mwaka huu.

Alibainisha kuwa kasi hiyo ya ongezeko la bei ilitokana na kupanda kwa bei za nishati, maji, makazi, usafirishaji, chakula na vinywaji visivyokuwa na kilevi.

Akizungumzia kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania kwa mwaka 2010, ilishuka kwa asilimia 8.5 hadi wastani wa shilingi 1,432.3 kwa dola moja ya Marekani kutoka wastani wa sh. 1,320.0 mwaka 2009.

Hata hivyo alisema kuwa thamani ya shilingi ilishuka kwa kiwango kidogo mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 10.4 mwaka 2009 na kueleza kuwa kushuka huko kwa thamani ya shilingi kulitokana na kuongezeka kwa mahitaji ya dola nchini pamoja na kuimarika kwa dola ya Marekani dhidi ya sarafu za mataifa mengine.

Kwa upande wa mapato ya ndani kwa kipindi cha mwaka 2009/10 yaliongezeka hadi kufikia asilimia 8.2 lakini kiasi kilichokusanywa ni pungufu ya makadirio kwa asilimia 8.8 kwa mwaka huo wa 2009/10.

Alisema kuwa wastani wa makusanyo kwa mwezi uliongezeka kutoka  wastani wa sh. milioni 357.8 kwa mwezi mwaka 2008/09 hadi  sh. bilioni 388.5 kwa mwezi mwaka 2009/10 na sh. bilioni 473 kwa mwezi  kwa miezi tisa ya mwaka 2010/11.

Katika kipindi cha Julai 2010 hadi Machi 2011 mapato ya ndani  yakijumuisha mapato ya halmashauri yalifikia sh. bilioni 4,256.3 ikiwa ni sawa na asilimia 31 chini ya lengo la bajeti ya mwaka 2010/11 ambalo ni sh. bilioni 6,176.2.

Akizungumzia misaada ya nje katika mwaka wa 2009/2010 ilikuwa ni sh. bilioni 1,405.3 ikilinganishwa na matarajio ya sh. bilioni 2,090.9 katika kipindi hicho lakini kwa kipindi cha Julai 2010 hadi Machi 2011 jumla ya misaada na mikopo ya kibajeti ilikuwa sh. bilioni 845.7 sawa na asilimia 3 zaidi ya makadilio ya bajeti.

Kwa upande wa matumizi ya serikali yalifikia sh. bilioni 8,173.7 mwaka 2009/10 sawa na asilimia 92.0 ya makadirio ambapo alisema kuwa kati ya fedha hizo matumizi ya kawaida yalikuwa sh. bilioni 5,562.4 na ya maendeleo yalikuwa sh. bilioni 2,611.3.

Hata hivyo, alibainisha kuwa hadi kufikia Desemba mwaka jana deni la Taifa lilikuwa limefikia dola za Marekani milioni 11,380.2 ikiwa ni ongezeko la dola milioni 654.28 ikilinganishwa na deni la kipindi  kama hicho mwaka 2009.

Alibainisha kuwa ongezeko hilo lilitokana na mikopo mipya ya ndani na nje yenye masharti nafuu kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Malipo ya deni hilo la Taifa katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka ulioishia Machi mwaka huu yalikuwa sh. bilioni 803.64.

Alisema kuwa katika suala zima la kutoa msukumo wa utekelezaji na ufuatiliaji wa kuhakikisha uchumi unakua yapo mambo muhimu mbalimbali ambayo serikali itayafanyia kazi katika kipindi cha mwaka 2011/2012.

Alisema kuwa serikali itaongeza msukumo katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya maendeleo ya 2025, kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kukuza pato la Taifa, kuongeza uwekezaji katika maeneo ya kimkakati na yenye mwingiliano kisekta hususani umeme, bandari, reli, maji na chakula cha hifadhi na kuhimiza ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo.

Hatua zingine ni kutumia fursa ya nchi kuwa kiungo muhimu kibiashara na nchi zinazotuzunguka ambazo hazina bandari, kuhimiza na kuhamasisha utekelezaji wa kilimo kwanza, kujizatiti katika kuboresha mazingira ya bishara na kuongeza usimamiaji wa mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi na kuimarisha usimamizi katika matumizi ya fedha za umeme.

No comments:

Post a Comment