Na Agnes Mwaijega
MBUNGE wa Korogwe Mjini, Bw. Yusuf Nasri amejitetea mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kuwa fomu za matamko ya mali alizijaza, isipokuwa
ofisi ya masijala ina mapungufufu makubwa katika suala utunzaji wa fomu hizo.
Mbunge huyo ni miongoni mwa viongozi wa umma ambao wameitwa na baraza la maadili Dar es Salaam jana kutokana na fomu yake ya tamko juu ya mali anazomiliki kutokuwepo tume ya maadili.
Mbunge huyo alidai mbele ya baraza hilo kuwa alijaza na kuzipeleka fomu hizo katika ofisi ya masijala mjini Dodoma Desemba 22, mwaka jana lakini anashangaa kuitwa kuhojiwa.
"Nilitimiza wajibu wangu kama kiongozi ambaye ninafahamu sheria na taratibu, upungufu wa kimasijala ndiyo uliyosababisha mimi kuwepo hapa leo," alisema.
Alisema ili kukabiliana na tatizo la fomu kutokuonekana wakati zimeshajazwa ni lazima tume ya maadili iweke taratibu za kuboresha masijala yake.
Hata hivyo, sekretarieti ya maadili ilidai kuwa orodha zao zinaonesha kuwa Bw. Nasri hakuwasilisha fomu hizo kwa wakati kwa hivyo hana tofauti na wale ambao hawajawasilisha.
Kwa upande wa Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Usevia Wilaya ya Mpanda, Bw. Vultana Kundy alijitetea kuwa fomu za matamko ya mwaka 2008 hakupata, na za mwaka 2009 alijaza na kuzirudisha ofisi ya maadili.
Sekritarieti ya maadili ilisema utetezi wake hauna mantiki kwa sababu ameshindwa kuonesha nakala ya fomu anayodai kuwa alijaza na kuirejesha katika ofisi ya maadili.
No comments:
Post a Comment