21 June 2011

Wabunge walia faini makosa ya barabarani

Na Grace Michael, Dodoma

MJADALA wa Bajeti ya Serikali jana uliendelea bungeni huku wabunge wakijikita kujadili vipaumbele vilivyoainishwa kwenye bajeti hiyo huku wakipinga baadhi ya
vyanzo vya mapato kama kuongezeka kwa faini za makosa barabara.

Suala la kuongezwa kwa faini za makosa barabarani lilionekana kuwagusa wabunge wengi ambao walisema kuwa serikali inatakiwa kuliangalia kwa makini kwa kuwa linalenga kuumiza wananchi badala ya kuwasaidia huku likiibia tatizo jingine la rushwa.

Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Njombe Kaskazini, Bw. Deo Sanga (CCM), alisema kuwa kupandisha faini hizo si njia sahihi ya kutatua tatizo la usalama barabarani bali itasababisha matatizo kwa wananchi na kuongeza mianya ya rushwa.

“Ni lazima hapa serikali iangalie kwa makini na ikibidi hata kujifunza nchi zingine kwani haiwezekani makosa yaanzie sh. 50,000 hadi 300,000 hapa tutawaumiza wananchi wetu na si kuwasaidia,” alisema Bw. Sanga.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Bi. Rose Kamili (CHADEMA) alipingana na hoja hiyo akisema kuwa endapo faini hiyo haitapunguzwa kutoka hapo ilipokadiriwa basi, serikali itakuwa imezalisha tatizo jingine la rushwa kwa kuwa hata hicho kiwango cha awali cha sh. 20,000 kilikuwa kikiwasumbua wananchi.

Kutokana na hali hiyo, wabunge walishauri kuondolewa kwa kiwango hicho kilichopendekezwa ili kibaki cha awali na kuhakikisha sheria za usalama barabarani zinafuatwa.

Akichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Mtera, Bw. Livingstone Lusinde (CCM), alisema kuwa tatizo kubwa lililopo ni utekelezaji wa vipaumbele ambavyo vimekuwa vikiwekwa kwenye bajeti.

Alisema kutokana na kutosimamia vyema vipaumbele maeneo mengi hasa ya vijijini yamejikuta yakikosa huduma muhimu za kijamii kama maji, umeme, miundombinu, afya na zingine.

Akichambua vipaumbele hivyo kwa kuanza na miundombinu alisema kuwa kutokana na kushindwa kuweka vipaumbele katika maeneo mengine, Dar es Salaam imejikuta ikiwa na tatizo kubwa la msongamano wa magari barabarani kwa kuwa miundombinu iliyopo
sasa inashindwa kukidhi mahitaji.

“Nadhani kwa kutozingatia masuala mengi au kusahaulika kwa baadhi ya maeneo ndiko kunachangia hata serikali yetu kukwama kuhamia hapa Dodoma na ingekuwa vyema sasa Spika angeanza kuhamia hapa kwa kuwa hakuna kinachomfanya abaki Dar es Salaam wakati bunge liko Dodoma,” alisema Bw. Lusinde.

 “Viongozi kukaa Dar es Salaam kunawafanya washindwe hata kutekeleza majumu yao kwa kuwa muda mwingi wanautumia barabarani na wakifika ofisini tayari wanakuwa wamechoka na wanachokifanya ni kunywa chai na kusoma magazeti, na ndio maana kazi ya kutekeleza mipango ya serikali haifanikiwi,” alisema Bw. Lusinde.

Alisema kutokana na hali iliyopo, mambo mengi yamekuwa yakifanywa bila kuangalia athari zake ambapo alitolea mfano wa matangazo ya biashara ya pombe kwenye vyombo vya habari ambayo alisema yamekuwa yakilitesa taifa hivyo akataka matangazo ya aina kama hiyo yakataliwe.

“Mfano umekaa kwenye TV na uko na masheikh, maaskofu unaona linapita tangazo la Safari Lager urithi wetu. Hivi kama urithi wa nchi utakuwa pombe, hali ya nchi yenyewe itakuwaje na ndio maana wakati mwingine hata mijadala yetu inaendeshwa kama tumelewa,” alisema

Kwa upande wa Mbunge wa Ilemela, Bw. Highness Kiwia (CHADEMA), alisema kuwa pamoja na baba wa taifa kupambana na ukoloni lakini ukoloni huo kwa sasa umerejea kwa sura mpya ya ufisadi ambao Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere alisema ni adui mkuu wa maendeleo kuliko hata vita.

Akizungumzia umeme, alisema kuwa wananchi wa Ilemela wamechoshwa na nyimbo za Waziri wa Nishati na Madini ambazo kila ziku zinaelezea utekelezaji wa miradi yenye megawati kadhaa katika maeneo mbalimbali kupata umeme wenyewe.

5 comments:

  1. Kweli faini ya elfu hamsini ni kumuumiza mwananchi.
    Kupandisha kiwango cha faini kuwa juu sio njia muafaka ya kupunguza makosa ya usalama barabarani. Wala kiwango cha faini kinacholipwa kwa serikali kisichukuliwe kama ni pato la serikali.Sasa mara nyingi tumekwisha shuhudia polisi wakitangaza viwango mbalimbali vya fedha walizoingiza kutokana na makosa hayo na ikachukuliwa kuwa ni ufanisi mzuri. Ndiyo maana naamini kuwa pendekezo la kupandisha kiwango hicho cha faini limelenga mapato zaidi, lakini sio kuondoa tatizo. Wabunge mliochangia hili hongereni sana, Polisi wanapaswa kutumia sheria zilizopo kuhakikisha kuwa usalama barabarani unakuwepo. Kwa mfano iwapo dereva ni mkorofi badala ya kumuandikia hiyo faini wanaweze wakaandaa mashitaka na dereva akafikishwa mahakamani. Suala la dereva kufikishwa mahamani ni njia sahihi ya kumrekebisha derevakuliko kuandika faini ambapo sana anayeumia ni mmiliko wa gari na sio dereva.

    ReplyDelete
  2. Wakati mwingine unashindwa kuelewa muelekeo wa sera za CCM kama serikali. Mara nyingi sera za ukandamizaji wa wananchi zinaongezwa nguvu kuliko zile za kuboresha hali yao. Watu wamedai pensheni zao mpaka wanaaga dunia, hakuna wa kuwasikiliza. Watu wamedai nyongeza za mishahara mpaka wamekaukiwa mate, kimyaa! Kila mahali watu wananyang'anywa ardhi, wamebomolewa nyumba, mashamba n.k., hakuna mtetezi! Sasa hizi adhabu za barabarani za sh. 300,000/=, si tutafungana tu jamani? Hivi ni kwa kipato gani cha Mtanzania wa leo kinaweza kumfanya alipe hizo faini, hasa ukiangalia kwamba wengi wa wenye magari hayo wameyakopa tu? Au ndiyo mmedhamiria kunyang'anya kabisa na magari yenyewe? Mimi sijaelewa hivi vigezo vinavyotumika kupanga haya tunaangalia au kupima vipi, maana hata Mkullo mwenyewe hawezi kulipa hiyo faini! Aseme kama nadanganya!

    ReplyDelete
  3. Ikumbukwe kuwa kiasi kikubwa cha fedha za faini zinaishia mifukoni mwa trafiki na kingine kwa makamamba wanaowaweka trafiki hao barabarani! Kinachotakiwa ni kuweka utaratibu mzuri wa kulipa faini hizo na sio kuongeza maana kufanya hivyo ni kuongeza rushwa na kuwaumiza wananchi wa kawaida!!! Sheria inatakiwa kusimamiwa na sio kuongeza kiwango!!!

    ReplyDelete
  4. Nyinyi munalalamika kuwa makosa ya barabarani yamekuwa mengi sana, mfano kutanua hata mbele ya askari.

    Leo mumewekewa faini ili kupunguza hayo makosa munalalamika.

    Watanzania munataka nini hasa? Kama munaona faini kubwa basi jitahidini musifanye makosa ya kizembe.

    ReplyDelete
  5. wewe hapo juu huna maana kabisa! Nani kwakwambia fine kubwa ndo dawa! Naomba uwe mukweli, kwa fine hiyo laki tatu polisi watachukua tena hizo elfu 2, 5, au 10!, rushwa itaongezeka sana, hata walokuwa wanalipa zile elf 20, hawatalipa tena ila watatoa rushwa kwa polisi hata ya 50 au laki kuliko laki tatu. Tatizo siyo madereva peke yake bali pia miundombinu mibovu inashawishi watu kutenda makosa kila mara! Fikiria foleni ilivyondefu sababu ya barabara nyembamba na concentration ya offices city center na kariakoo, hapo mtu asifikirie kutanua! Naamini miundombinu ikiwekwa sawa, hiyo kutanua haitokuwepo. Haya, taa za magomeni, ubungo na mlimani city wakati mwingine hazina umeme au mbovu na hakuna traffic wa kuongoza magari, bahati mbaya watu wanagongana traffic akija anapima anasema driver X au Y ndo mwenye makosa, kumbe taa ndo tatizo! Tunalipa pesa nyingi sana za barabara kwenye kilaq lita ya petrol au diesel, tunalipa pia kodi mbalimbali kwa wingi but serikali hawatuboreshei miundo mbinu leo hii wanataka laki tatu, haya polisi wanagawa leseni ovyo nayo inachangia ajali sana tu. Cha muhimu hapa miundo mbinu iwe safi, polisi watoe leseni kufuata utaratibu, sheria pia zisimamiwe vizuri tatizo litapungua maana kuisha kabisa haiwezekani.

    ReplyDelete