07 June 2011

Mbowe Huru

*Asafirishwa kwa ndege ya JWTZ, abadilisha mdhamini

Na Waandishi Wetu, Arusha

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha imemwachia huru bila masharti Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Freeman Mbowe huku
ikitoa onyo dhidi ya wote wanaokiuka sheria halali zinazotafsiriwa na mahakama.

Kitendo hicho cha kumwachia Bw. Mbowe bila masharti magumu kama ilivyotarajiwa, iliwafanya wanachama na wapenzi wa chama hicho waliokuwa wamefurika mahakamani hapo kulipuka kwa furaha, na kuondoka kwa amani na kuwaacha walinzi waliokuwa wamejipanga  kukabiliana na lolote.

Mahakama hiyo chini ya Hakimu Mkazi, Bw. Charles Magesa ilifuta
udhamini wa aliyekuwa mdhamini wa Bw. Mbowe,  Bw. Isaya Margwe, na badala yake Mwenyekiti ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, kudhaminiwa na Msemaji wa chama hicho jijini Arusha,
ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Elerai (CHADEMA), Bw. John Bayo.

Hakimu Magesa alisema kuwa sheria zinamwagiza mdhamini kufika mahakamani siku ya shauri husika na kutoa taarifa zinazohusu mshitakiwa iwapo amepata udhuru, na si vinginevyo.

“Taarifa za udhuru zinatakiwa kufikishwa mahakamani na mdhamini
mapema kwa kuwa ni sheria, hata Juni 24 mwaka huu ambapo washitakiwa wanatakiwa mahakamani wadhamani wao wanatakiwa  kufika na kutoa tarifa juu ya washtakiwa hao na si vinginevyo, ama sivyo sheria itachukua mkondo wake,” alisisitiza Bw. Magesa.

Mahakama hiyo ilitoa masharti ya dhamana kwa Bw. Bayo sawa na yale yaliyotolewa awali kwa wadhamini wengine ya dhamana ya kuwa na fedha taslimu sh milioni 2 na kuwa mkazi halali wa Arusha, masharti ambayo yalifikiwa na mdhamini huyo na kuruhusiwa kumdhamini.

Awali, Wakili wa Utetezi wa kesi hiyo, Bw. Method Kimomogolo
aliambia mahakama kuwa watuhumiwa hao ambao pia ni wawakilishi
wa majimbo mbalimbali nchini wanaweza wasifike mahakamani hapo Juni 24, mwaka huu kutokana na vikao vya bunge vinavyoanza leo.

Kwa sababu huyo, wakili huyo aliiomba mahakama hiyo kuwa ni vema kama kesi hiyo ikaahirishwa hadi September 7, mwaka huu vikao vya mbunge vitakapokuwa vimefikia tamati, lakini ombi lake lilikataliwa na mahakama hiyo.

Akizungumzia hoja hiyo, Wakili wa Serikali, Bw. Juma Ramadhani  alisema kuwa kwa kuwa kesi hiyo ni ya jinai ni vizuri mahakama ikaisikiliza mapema na kwa mapana zaidi, hivyo si vema kuahirishwa mara kwa mara.

Kauli ya Mbowe

Akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kudhaminiwa, Bw. Mbowe alisema ni vizuri serikali ikawa makini na matumizi makubwa ya fedha za wananchi kwa kuwa na mahesabu maalumu ambayo yataweza kusaidia jamii kukabiliana na makali ya maisha na kuepuka kutumia fedha nyingi kwa matumizi yasiyo ya lazima.

“Mimi kuletwa hapa na vyombo vya usalama imetumika gharama kubwa
sana wakati serikali haina fedha kwa ajili ya vitengo vyake. umefika wakati wa serikali kuafikiria hili,” alisema Bw. Mbowe.

Alieleza kuwa alisafirishwa alfajiri jana kutoka Dar es
Salaam kwenda Arusha kwa kutumia Ndege ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kupokelewa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ambapo alisindikizwa na vyombo vya dola kwa gharama kubwa, kitu alichosema hakiinufaishi jamii inayokabiliwa
na changamoto nyingi za uhaba wa fedha na matatizo mengineyo.

Kauli ya Polisi

Jeshi la Polisi limesema halitamwogopa kiongozi yeyote wa ngazi ya juu kumchukulia hatua za kisheria pindi anapokwenda kinyume.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Kamishna wa Operesheni wa Jeshi hilo, Bw. Paul Chagonja huku akisisitiza kuwa hawakumdhalilisha Bw. Mbowe bali amefanya hivyo mwenyewe kwa kukiuka amri ya mahakama.

Alisema jeshi hilo linafanyakazi kwa mujibu wa sheria za nchi hivyo halitakwenda kinyume na sheria kutokana na kitendo cha mtu mmoja chenye nia ya 'kuwania madaraka kwa nguvu'.

"Nasema hivi, kukamatwa kwa Mbowe ni sahihi kwani tumefuata amri ya mahakama ambayo Mbowe ameshindwa kuitekeleza.

"Kama mtu anawania madaraka kwanini asisubiri mwaka 2015 ili aweze kupata nafasi hiyo kuliko kuchochea vurugu na kusababisha vifo," alisema Kamishna Chagonja.

Bw. Chagonja alisema jeshi hilo halitavumilia kutokea kwa vifo vya Watanzania kama ambavyo vilitokea mkoani Arusha  wakati wanasambaratisha na maandamano ya CHADEMA na maeneo mengine.

"Mwananchi akijaribu kushiriki kwenye maandamano ambayo hayana kibali na kukamatwa atakayepata shida ni familia yake na hakuna kiongozi yeyote atakayemsaidia kulisha familia," alisema.

Walioandamana Dar kortini

Wanachama watatu wa CHADEMA wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za kuandamana bila kibali na kusababisha uvunjifu wa amani.

Wanachama hao akiwamo Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la chama hicho, walikamatwa wakati wanaandamana Dar es Salaam kushinikiza kuachwa huru kwa Bw. Mbowe juzi jioni.

Mwendesha Mashtaka, Bi. Elizabeth Kaganda alidai mbele ya Hakimu Sundi Fimbo kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo Juni 5 mwaka huu eneo la Ufipa Kinondoni.

Washtakiwa hao ni Bw. Jeneral Kadumu, Bw. Juliana Daniel na Bw. Joseph Msetti ambapo wakishilikiana na wenzao ambao hawajafahamika, pia walitenda kosa la kula njama ya kutenda kosa hilo.

Bi.Kaganda alidai kuwa siku ya tukio  saa 11 jioni katika eneo la Magomeni washitakiwa hao walifanya mkusanyiko na kuandamana bila kibali kitendo kilichosababisha uvunjifu wa amani kwa wakazi wa eneo hilo.

Washtakiwa ambao wanatetewa na Wakili Mabere Marando walikana kutenda kosa hilo na upande wa mashatika ulidai kuwa upelelezi wa kesi bado haujakamilika, na dhamana yao ilikuwa wazi, endapo wangetimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili wanaofanyakazi katika kampuni zinazotambulika ambao watasaini hati ya sh. milioni nne.

Washitakiwa hao walikuwa na wadhamini hao lakini upande wa mashitaka uliiomba mahakama iwape siku moja ili waweze kupitia na kukagua barua za wadhamini kwa kuwa kipindi hiki kumekuwapo na wadhamini waongo.

Kesi iliahirishwa hadi leo kwa ajili ya kutoa dhamana.

7 comments:

  1. Mkitaka siasa jifunzeni Z'bar! Joto, kishindo, tafrani, heka heka, matusi, mawe leo hii kimyaaaaa kama hakuna alopigwa virungu! Siasa ni ulaji tu na blah blah

    ReplyDelete
  2. Yote haya ni mbinu za CCM kutaka kukwamisha mafanikio ya chama cha chadema.Mahakama na polisi ni vyombo vya kuhakikisha amani inakuwepo kwa wananchi lakini sio kuwasumbua watetezi wetu sisi wananchi tunao kandamizwa na mafisadi.hawa mafisadi pamoja na raisi wao wajifunze kutoka kwa viongozi wa chadema jinsi wanavyo tetea haki zetu wanyonge.mfano tosha watanzania wajaribu kutathimin tukio la mgodi wa north mara.ccm ni ya kufa tu watu wake na raisi wao wajiandae kubeba virago vyao 2015.

    ReplyDelete
  3. kamishna paul chagonja anataka kuingia kwenye list ya ocampo moreno....HANA AKILI MPUMBAVU MKUBWA!- -- hivi hakuna sheria ya kufungua kesi mahakamani dhidi yake??

    ReplyDelete
  4. chagonja amezoea rushwa ndiyo maana ana kitambi, hivi kweli wakitaka kushindana mbio za marathon chagonja na mbowe nani atashindwa? chagonja atahemea kifuani amejaa mafuta ya wizi; hata kutamka arrest hajui

    ReplyDelete
  5. Tusitambe kuwa CCM itangoka mwaka 2015. Wakifanya kamchezo kama ka mwaka jana?
    La muhimu ni kuandaa mapema katiba itakayoweka mazingira huru ya uchaguzi. Tume huru ya uchaguzi isichaguliwe na Rais. Utaratibu mbadala uwekwe. Vinginevyo ndugu zangu kamchezo ka 2010 katarudiwa na mtabaki midomo wazi!

    ReplyDelete
  6. Wakifanya kamchezo ka 201 uchaguzi wa 2015 Tanzania itageuka Libya. Tutaitetea haki yetu ikibidi tutakufa kishujaa.Chagonja anaonesha anashabia chama flani.Kwani kulikuwa na ulazima gani wa kuzungumzia kuhusu uchaguzi 2015 au kuchukua madaraka kinguvu? Siku zake zinahesabika, CHADEMA tukikamata dola 2015 atakufa kwa presha.

    ReplyDelete
  7. huyo polisi gani ana kitambi, kazi unafiki tu.Nadhani katumwa

    ReplyDelete