06 June 2011

Kukamatwa Mbowe balaa tupu Dar

*Wafuasi waandamana, watawanywa, watatu mbaroni
*Dkt. Slaa asema 'ukondoo' wao umefika kikomo
*CUF waungana na CHADEMA, watangaza maandamano


Na Benjamin Masese

Kauli ya Dkt. Slaa

CHADEMA kimesema kuwa 'ukondoo wao' na uvumilivu dhidi ya udhalilishaji na unyanyasaji unaofanywa na jeshi la polisi kwa viongozi na wabunge wake
umefikia kikomo na sasa kitaanza kufanya maamuzi mazito muda wowote.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dkt. Willibrod Slaa alisemsa hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kulaani kitendo cha polisi kumshikilia Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Freeman Mbowe huku wakijua wazi ndiye Waziri Mkuu Kivuli na mwakilishi wa Kambi ya Upinzani kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge inayotrarajia kukutana leo Dodoma.

Dkt. Slaa alisema kuwa uvumilivu wao umefikia mwisho wa kuona serikali kupitia Jeshi la Polisi ikiendelea na mkakati wa kuwadhalilisha na kuwadhoofisha wabunge na viongozi kwa kuwakamata bila kufuata taratibu husika, tofauti na wenzao wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alisema kutokana na hali hiyo CHADEMA kimetoa maazimio yao kwamba muda wowote kinaingia barabarani kuidhabu serikali kwa kutumia nguvu ya umma, ikiwa Bw. Mbowe ataendelea kushikiliwa na kushindwa kuhudhuria vikao vya bunge.

Pia alisema kuwa wabunge wote wa CHADEMA hawatashiriki katika bunge lijalo na hata vikao vinavyoanza leo mkoani Dodoma.

Dkt. Slaa alisema chama hicho kisitupiwe lawama ikiwa machafuko yatatokea nchini bali lawama zielekezwe kwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na jeshi lake la polisi na taarifa tayari zimefikishwa sehemu zote husika ndani na nje ya nchi.

Alisema kuwa kitendo cha serikali kudai kwamba CHADEMA inaendesha uchochezi unaohatarisha amani nchini katika mikutano yao si kweli, bali imeona chama hicho kinatoa elimu kwa wananchi ili kujua haki zao ndio maana imeanzisha mkakati wa 'kamata kamata na dhalilisha'.

Dkt. Slaa alisema hivi sasa anaendelea na mawasiliano na viongozi wa Chadema katika mikoa yote nchini ili kujipanga kuiadhibu serikali kwa kuwa tangu matukio yatokee hakuna kauli yoyote ilitolewa na Rais Kikwete au Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda kuomba radhi au kutoa pole kwa mauaji yalitokea mkoani Mara.

Wakati mkutano huo ukiendelea tayari mamia ya vijana walikuwa wamejikusanya makao makuu ya chama hicho wakisubiri kupewa amri ya kuingia barabarani lakini Dkt. Slaa aliwaomba kuwa na subira ili kuimarisha mawasiliano sehemu zote za nchi.

"Napigiwa simu na RCO kila mara akinitaka kuwatuliza vijana wangu ambao wengine tayari wamefika kituoni lakini ninachomueleza na kumsisitizia ni kwamba ninaendelea kuwasiliana na wengine nchi nzima ili kuongeza nguvu... na hili tusilaumiwe kamwe," alisisitiza na kushangaliwa na vijana wakitaka kupewa ruksa muda huo.

Baadhi ya viongozi wa chama hicho na upinzani walifika katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam anakoshikiliwa Bw. Mbowe ili kujua hatma yake na kufanya kikao na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Bw.  Suleiman Kova.

Waliofika hapo ni Mbunge wa Ubungo, Bw. John Mnyika, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na wengine ambao walitoa mapendekezo yao.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka kwenye kikao hicho, Profesa Lipumba alisema kuwa lengo la kufika hapo ni kutaka kumwekea dhamana Bw. Mbowe kwa kuwa ni tegemeo lao katika Kambi ya Upinzania na hasa bunge lijalo.

"Nimestushwa sana na kitendo cha Mbowe kukamatwa kipindi hiki wakati akiwa katika maandalizi ya hoja za Bunge la bajeti, na hii ni kuminya demokrasia, na kitendo cha kuendelea kumshikilia kinaongeza hasira ukizingatia hivi sasa hakuna heshima tena kwa wabunge wa upinzani, isitoshe spika yupo kimya, hatukubaliani na hili," alisema.

Alisema kuwa wapinzani watakutana muda wowote ili kutoa tamko la pamoja kwa kuwa tayari imeonesha wazi sheria hazifuatwi katika kesi hii badala yake siasa zimechukua nafasi kubwa.

"Kuna wezi wa mabilioni wanatembea barabarani hadi sasa na hawakamatwi na polisi, lakini jeshi la polisi limeonekana kufanya oporesheni ya kuwamakata wabunge, sasa tunaondoa tofauti zetu na sasa tunaungana kupinga vitendo hivi," alisema.

Naye Bw. Mnyika alisema katika kikao hicho walimuomba Bw. Kova kuwa hakuna sababu ya kumpeleka Bw. Mbowe Arusha, aachiwe huru ili ahudhuria bungeni, na kama anapelekwa asipelekwe chini ya ulinzi kwa kuwa wananchi wanaweza kusababisha machafuko.

Hata hivyo, alisema licha ya mazungumzo yao ya muda mrefu na Bw. Kova, afande huyo alisisitiza kwamba polisi kama chombo cha ulinzi kinatekeleza amri iliyolewa na mahakama.

Bw. Kova alilieleza majira  kuwa jeshi la polisi limejiandaa kumpeleka Bw. Mbowe mkoani Arusha muda wowote ili kufikishwa mahakamani leo.

Alisema kuwa taratibu za kumsafirisha zimekamilika na kutoa mwito kwa wananchi kuwa watulivu na kuiachia mahakama ifanya kazi zake.

Bw. Kova alisema kuwa jeshi la polisi halina nafasi ya kujadilia amri ya mahakama, hivyo lazima Bw. Mbowe afikishwe mahakamani na tayari ulinzi umeimarishwa hapo Arusha.


Kauli ya Chadema Mara

Mwandishi wetu Hellena Magabe anaripoti kutoka Musoma kuwa Chadema mkoani Mara imesema kufikia leo saa nne asubuhi inataka kumwona Bw. Mbowe ameachiwa huru bila masharti yoyote.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mara, Bw. Charles Kayere alisema wanamtaka Spika wa Bunge atoe tamko juu ya kinga ya wabunge kukamatwa ovyo ovyo na kudhalilishwa, hasa wale wa upinzani.

Alilaani kitendo cha polisi kumkamata kiongozi huyo siku ambazo si za kazi ili asote mahabusu, akisema ni cha kinyama na kitasababisha uzalendo uwashinde.

Aliongeza kuwa mahakama imekuwa ikitaja kesi hiyo ovyo kabla ya upelelezi kukamilika, jambo ambalo linawatia mashaka kuwa hujuma inafanyika ili kuwadhalilisha wabunge hao wa Chadema.


CUF kupinga kwa maandamano

Chama cha Wananchi (CUF), kimetangaza kufanya maandamano ya amani kupinga udhalilishwaji wanaofanyiwa wabunge kwa kukamatwa wakiwa katika majukumu yao na mauaji ya
raia wasiokuwa na hatia unaofanywa na Jeshi la Polisi nchini.

Kaimu Naibu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa mipango, uchaguzi na Bunge, Shaweji Mketo, alisema jana kuwa chama hicho kitafanya maandamano Juni 12, mwaka huu yakiongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba.

Alisema maandamano hayo yatakayoanzia Ubungo Mataa na kuishia katika viwanja vya Manzese Bakharesa kwa mkutano wa hadhara utakaohutubiwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho ngazi ya taifa.

Mketo, alisema Jeshi la Polisi hivi sasa limekuwa likiwadhalilisha wabunge na kuwaua wananchi wasio na hatia hasa pindi wanapokuwa wanadai haki zao za kimsingi kwa mujibu wa katiba ya nchi.

“Sote tumekuwa mashahidi kwa hili raia wanauawa na polisi bila hatia, lakini bado kumekuwa na tabia iliyojengeka ya
kuwadhalilisha wabunge hasa kutoka vyama vya upinzani. Huu ni udhalilishaji wa hali ya juu na tunawaomba wanaharakati  na wananachi wote kwa ujumla watuunge mkono kwa hili,” alisema Mketo.

Aidha CUF imelaani kitendo cha polisi kuwakamata waandishi wa habari wakiwa katika majukumu yao ya kazi katika Kijiji cha Nyamongo, wilayani Tarime kwani si kitendo cha kiungwana na kinakwenda kinyume cha katiba na tamko la haki za binadamu ambalo Tanzania imeridhia.

Alisema kitendo cha kuwakamata wabunge hao ni udhalilishaji wa wazi na kutoheshimu hadhi ya mbunge na madaraka ya bunge.

Wabunge waliokamatwa ni pamoja , Bi Magdalena Sakayana (Viti Maalumu-CUF_, Bw. Tundu Lissu (Singida Mashariki-CHADEMA), Bi. Ester Matiko (Viti Maalumu-CHADEMA) na Kiongozi wa Kambi ya upinzani Bungeni, Bw. Freeman Mbowe-CHADEMA.

Pamoja na hatu hiyo alisema CUF inalaani kitendo cha Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwanyima dhamana wajumbe wake wa Baraza Kuu akiwemo Zainabu Nyumba, ambaye ni mlemavu wa ngozi (albino).

Alisema mbali na kuwanyima dhamana viongozi hao, Jeshi la Polisi limeendelea kuwakatama wananchi katika Jimbo la Urambo Magharibi na kufikia 30 hadi kufikia juzi.

17 comments:

  1. kilichobaki ni nguvu ya uma kutumika na hao polisi ni kua tunawaheshimu sio kua wanatushinda wasubiri siku tunaanza kuwaadhibu watakoma.

    ReplyDelete
  2. hakuna haja ya kuoooooongeasaaaaaaaaaaaaaana ingieni mtani nn kinacho wafanya mshindwe kila siku mnatishia tu kelelenyingiiiiii ingieeeeeeni sasa hivi sio tu wakati wowote we mzeeeeee

    ReplyDelete
  3. Hivi hawaoni yanayotokea katika Ulimwengu wa Waarabu? Nguvu ya umma haizuiwi na bunduki!

    ReplyDelete
  4. Nguvu ya umma kwa upumbavu wa mtu mmoja asiyetaka kufuata sheria ndiyo atuingize vitani??? alitakiwa kwenda mahakamani hakwenda wenzie walikwenda akapewa nafasi ya pili hakwenda akidai hawezi kupiga magoti hivi nchi hii imekuwa ya kihuni kiasi hicho? huyu ni DJ arudie kazi yake mambo mengine hayawezi, Serikari ipo kusimamie sheria kanuni na taratibu (STK) sasa wamemvumilia wamechoka amepata alichokitaka, mnaotaka kuingia mitaani jaribuni,kama mnaona ya misri na libya nimazuri yakuiga mtakipata mnachokitafuta
    Mbowe hawezi kutusababishia vurugu nchini, ingelikuwa ni amri yangu angesahaulika lupango

    ReplyDelete
  5. Wapinzani ndo watetezi wetu . Kumkamata kiongozi wa upinzani ili asishiriki bajeti ni kuandaa mwanya wa kupitisha madudu.
    Tunakoelekea si kuzuri. Upinzani si uadui ni fursa ya kuikosoa serikali. Vita ikilipuka serikali ilaumiwe maana inaandaa mazingira ya vita kwa kuwatumia polisi.

    ReplyDelete
  6. zote hizo njama wapinzani wasiingie bungeni kesho,wanatafuta mbinu chafu,lakini yote tisa,kumi tusubiri waanza kesho,waipate bajeti ya zitto,watakoma ubishi,maana nchi hii wanataka kuiserebusha kama ngoma

    ReplyDelete
  7. Ni kweli zote hizo njama za kuzuia wabunge wa vyama pinzani washindwe kushiriki kikao cha bajeti, Kwani wanajua kama wao ndo wanaowaweka wananchi wazi kila kitu.

    ReplyDelete
  8. Hebu ee niambieni nguvu ya Umma mnayoizungumzia ni ipi? Ni Chama fulani cha upinzani au vyama kadhaa au chama kilichomo madarakani? Watanzania wenzangu tuwe macho kuona kilicho sahihi kwa ajili yetu na nchi yetu. Tena haina maana yoyote kulinganisha hali ya nchi nyingine, ila tuangalie lile liwezalo kutuletea mema. Polisi waachiwe kufanya kazi zao zihususo usalama wa kila mtu. Mheshiwa Mbowe kupelekwa Arusha kwa ndege ni moja ya kulindwa kwake ili kama kutatokea jitu lisilo na hekima liwe la CCM au .... asalimike na umma pia. Kama angelifika mahakamani au mwakilishi wake jambo hili lisingelitokea. Dr Slaa kumbuka ya kwamba wewe ulikuwa Mtumishi wa Mungu na kiongozi "Usiushinde ubaya kwa kutumia ubaya bali uushinde ubaya kwa kutumia wema" Usiwapandie Watanzania moyo wa chuki ili wachukiana ukisema ukondoo wa chama umefikia kikomo! Mmmmmmmmmmmmmmmmm! Nawaheshimu viongozi wote wapenda amani na nchi yetu. Hivi kweli Watanzania mnapenda tuuane?

    ReplyDelete
  9. Watanzania msiwe wapumbavu kiasi hicho ccm ni wauwaji wakwanza tanzania tena wameona chadema wamekuwa wapole ndiyo maana wanatunyanyasa. wanataka kumfanya Mbowe kama Kiiza Besigye wa Uganda? sisi tupo nje ya nchi yatanzania tuna aidi tutapambana hata kuingia msituni.ilitupatehaki yetu.na tunaomba Mbowe achiliwe mara moja iwezekanavyo kwani anamajukumu mengi Bungeni.

    ReplyDelete
  10. Viongozi wameshiba na sasa wanatamani kutapika,hizo pesa mlizoiba mtazikimbia,mnazidi kututia hasira,msione tumelala tunatunga sheria,Kikwete una lako jambo,walibya walikuwa na raha zaidi yetu, mishahara walikuwa wanalipwa wananchi wote,barabara zote lami,nchi ni jangwa lakini wanamwagilia,sisi chama cha majambazi,kinatuibia kila kitu,madini na mchanga wake wanausomba,pesa za umma unaziiba,sasa mmechoka kuiba,mmeanza kutoa roho za watu,kumbukeni kuwa siku hizi Mungu anatoa adhabu hapa hapa duniani,acheni kutesa watu.Mwachieni Mbowe,mwachieni,litakapo tokea la kutokea mtasahau hata chupi zenu,mnanitia hasira,watanzania tumelogwa?

    ReplyDelete
  11. Haipendezi ,naona sasa hili ni sikio la kufa kwa viongozi wa serikali ya awamu hii ya nne ,baada ya kuwakamata majambazi ,mafisadi mmeamua kuwakamat watetezi ,wazalendo.jambo hili linatukera ,kimtazamo haraka haraka tu ,hatuelekei kutatua matatizo yetu bali ni kuyapalilia ,ni wakati wetu sasa kupambana ili haki zetu watanzania ziheshimiwe,maendeleo ni haki yetu ya msingi ,hatuwezi kuendelea hata kidogo hali ikiwa ndio kama hii.Huu ububu mpaka lini.Tuamke watanzania

    ReplyDelete
  12. HIVI MBOWE NA CHADEMA NI ABOVE THE LAW? MAANA YEY NI MBUNGE NA ANJUA MIHILI YA DOLA ILIVYO,KAMA MAHAKAMA IMEKUITA UKAJITETEE KWANINI UNAOGOPA?ANATAFUTA HURUMA YA NANI?

    Baker Souza<DSM

    ReplyDelete
  13. wameshindwa kukamata mafisadi,wezi wa pesa umma,mafisadi wa rada ,wa richmond, wanakamata wapinzani, kazi hawana,wanatafuta deal kwa wapinzani,hilo ndege lote la nini kama alikuwa mtuhumiwa angesafirishwa na lory hata la jeshi usiku kucha,then asubuh anaamkia mahakamani,mbona wakatumia ndege na ulinzi,wanaonyesha walivyo na akl mgando,kumbe wapinzani ni watu makini ndo maana akapewa heshima hadi ulinzi.wangekamata mafisadi hivyo,nchi hii ingekuwa na heshima,wananchi wangewaheshimu.ndo maana mkatupiwa maweeeeeeeeeee.

    ReplyDelete
  14. maafande si wanavua magwanda wakifika nyumbani dawa ni ngumi za kuvizia kama kujidai kwao ni silaha walizonazo.

    kwa tabu mnazotupa tukiandamana mnatufundisha mbinu.SIKU INAKUJA.
    WAKUJILIPUA WALIANZAJE

    ReplyDelete
  15. serikali naona imeshindwa la kufanya kwani badala ya kuangalia mambo ya msingi ya kuboresha mahitaji muhimu kama barabara, maji na hospitali wanahangaika kumsakama kiumbe mpenda maendeleo anayesema ukweli wa mambo Mr Mbowe kwa lengo la kumdhalilisha na ili wananchi tuone kwamba hafai, mimi nasema hongera sana Mbowe kwa ujasiri wako na wanalolitafuta CCM hawalipati ng'o.Tupo na wewe daima na tunakupenda sana achana na hao wanata kukuharibia.hata wakufunge imani ya sisi na wewe kuwa unafaa ipo tu.

    ReplyDelete
  16. Wanaomwona Mbowe ni yule DJ waliyekuwa naye mitaani wanachemsha!Mtu anapokuwa na Madaraka ya Kitaifa hata kama alikuwa mvuvi ule uvuvi haupo tena.Ujinga wetu ndio unaofanya mpaka hata hao Polisi wenu wanamdharau Mbowe na kumkamata bila kujali nafais aliyo nayo ambayo inaweza kusababisha maafa makubwa kwa kumdharau tu.ANGALIZO!
    Watanzania Tuheshimu nafasi aliyo nayo mtu.Tuache kuchezea mamlaka.Angalieni Marekani.Obama ni mtu mweusi aliyekuwa wanamdharau kwa rangi yake, lakini alivyokuwa Rais, Heshima imezingatiwa.Si yule Obama Mkenya tena.Nawaomba Polisi wetu hasa Chagonja aelewe kuwa Leo ni Kikwete, lakini kesho anaweza kuwa Mbowehuyu huyu anayemdhihaki na kumwona fala.sijui atakimbilia pori gani wakati huo!

    ReplyDelete
  17. kweli watanzania wengi hawana upeo wa kuona mbali wala kujua zaidi ya pale anapoambiwa na akina mbowe na wenzake. nashangaa tena nashangaa kuona idadi kubwa wakimtetea mvunja sheria za nchi tena alizozitunga mwenyewe halafu anazivunja hivi hivi...akitegemea watanzania wasio na uwezo wa kufikiria zaidin ya maneno yale anayoambiwa kumtetea.

    Mbowe na wenzake wanajua wanachokifanya, wanajua uwezo wa watanzania wengi wa kufikirian zaidi ya pale wanaposema n mdogo, hivyo wanachokifanya hata kama ni kinyume na sheria watatetewa tu...

    Huu ni ufinyu wa fikra na hakuna kitu kibaya duniani kama kuwa mtu wa kuburuzhwa na kukubali ndiyo mzee, ndiyo mzee bila kutafakari na kutafiti kwa kina na hatimaye kupata jibu sahihi nani mkosaji.

    Hivi woooooooooote mliomtetea mbowe, mlitaka amri za mahakama ziwaguse watoto wa walalahoi tu??????? na mbowe abaki akiikejeli serikali na watu wake!

    Enendeni mkatafakari badala ya kila kitu kukilaumu chaka tawala...mbowe ni naniiiiiiiiii, mbona ni sawa na vijiti vingine tu vinavyoweza kusogezwa pembeni tena kwa miguu na watu wakapita?

    Watanzania tusiwe wajinga wa kupandikizwa upumbavu kwa nakuchukua upambavu huo kama ulivyo bila kuufanyia uchambuzi...hatari, hivyo mnataka Mahakama sifanye kazi zake kwa vile Mbowe kakosea? hiyo ni tisa subirini 10 yenyewe ambayo ni kesi itakapoanza...hakuna cha mbowe wala Ndesa wote sheria ni msumeno hukata kwenda na kurudi...Alasiki

    ReplyDelete