21 June 2011

Bonga Star Search kuanza Julai 9

Na Anneth Kagenda

MASHINDANO ya Bongo Star Search (BSS), yamepangwa kuanza Julai 9 mwaka huu na yanatarajia kushirikisha mastaa zaidi ya 34.Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi
wa Benchmark Production Ritta Poulsen, alisema mashindano ya mwaka huu yatakuwa na mvuto wa aina yake kutokana na kwamba wanaoshiriki tayari ni mastaa, ambao waliwahi kushiriki miaka mitano iliyopita.

Alisema hivi sasa wapo kwenye maandalizi ambapo Juni 25, mwaka huu watayatambulisha mashindano hayo rasmi kwa kuwaonesha washiriki watakaoshiriki kinyanganyiro hicho.

"Tunategemea kuwa ushindani utakuwa mkubwa, lakini pia wenye changamoto nyingi na hatujajua wananchi na mashabiki wataupokea vipi na pia hii inatokana na kwamba hawa wanaoshiriki si wageni kwa Watanzania kwani waliwahi kushiriki," alisema Ritta.

Mkurugenzi huyo alisema washiriki wa BSS walipokea ushiriki huo kwa moyo mkunjufu kwa kujua kwamba nafasi hiyo ni adimu kwani ni jambo la kushangaza, kuona kwamba wameitwa kwa mara nyingine na kusema suala hilo limekuwa kama neema kwao.

Hata hivyo alitoa wito kwa wasanii hao kwamba wanatakiwa kufanya vyema, kujitangaza, kujituma na kuonesha umahiri wa hali ya juu kutokana na kwamba wamekaa mtaani hivyo wanajua matatizo yote yaliyoko huko na kusema kuwa nafasi hiyo haiwezi kutokea tena.

Washiriki hao wanatokea mikoa mbalimbali ikiwamo Arusha, Tanga na Dodoma.

No comments:

Post a Comment