21 June 2011

Ilala yang'ara Copa Coca-Cola

Na Addolph Bruno

MASHINDANO ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 Copa Coca-Cola, yameendelea kupamba moto ambapo katika michezo ya jana timu ya Ilala imeibuka na ushindi wa
mabao 2-1 dhidi ya Manyara.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam Manyara ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 48 kupitia kwa Hashim Hamis kwa mkwaju wa penalti.

Ilala ilicharuka na kujibu mapigo dakika ya 81 baada ya shambulizi kali na kufanikiwa kusawazisha bao hilo kupitia kwa Alfred Gerald kwa mkwaju wa penalti baada mabeki wa Manyara kucheza faulo eneo la hatari.

Timu hiyo ya Ilala baada ya kupata bao hilo iliendeleza mashambulizi langoni mwa wapinzani wao na kufanikiwa kupata bao la pili na ushindi dakika ya 88 na Abdallah Haji, ambaye naye alifunga mkwaju wa penalti.

Mchezo mwingine ulikuwa kati ya Tanga na Pwani ambazo zilitoshana nguvu kwa kushindwa kufungana uliopigwa katika Uwanja wa Tanganyika Peckers Kawe, Dar es Salaam.

Katika Uwanja wa Tamco, Arusha ilitoka sare ya bao 1-1 na Morogoro katika mchezo uliokuwa na ushindani mkali.

Morogoro ilikuwa ya kwanza kujipatia bao la ushindi dakika ya 9 kupitia kwa Hassan Hamad, huku Arusha ikisawazisha bao hilo dakika ya 23 kupitia kwa Joseph Methiew.

Hatua ya makundi ya michuano hiyo inatarajia kumalizika kesho, ambapo timu 16 zilizofanya vyema katika makundi zitaingia hatua ya robo fainali.

No comments:

Post a Comment