06 May 2011

Yanga kuchuja wachezaji kesho Jangwani

Na Elizabeth Mayemba

BENCHI la Ufundi la Yanga, kesho na keshokutwa linatarajia kufanya mchujo katika kikosi chake cha vijana chini ya miaka 17 na 23 kwa ajili ya kupata kikosi
kipya.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji wa klabu hiyo, Louis Sendeu alisema kupatikana kwa wachezaji wazuri katika kikosi hicho kutawasaidia kupunguza makali ya usajili kwenye timu yao ya wakubwa.

"Kesho na keshokutwa benchi la ufundi litakuwa na kazi ya kufanya mchujo wa wachezaji watakaojitokeza na wale wa zamani kwa ajili ya kupata kikosi kipya, ambapo pia tunaamini hata kwenye timu ya wakubwa tunaweza kupata wachezaji kutoka huko kwa vijana," alisema Sendeu.

Alisema kazi hiyo ya mchujo wa wachezaji itafanywa na Kocha Felix Minziro na Meneja wake Keneth Mkapa, ambapo pia wanatarajia kupata wachezaji kutoka mikoani wenye vipaji.

Sendeu alisema pia wana mpango wa kupita na kwenye shule za vipaji kwa lengo la kupata wachezaji wazuri, ambao wataitumikia klabu hiyo na timu ya taifa.

Katika hatua nyingine, uongozi wa klabu hiyo umesema umeamua kuwasajili wachezaji wake Athuman Idd 'Chuji' na Shamte Ally baada ya kuona wananyemelewa na mahasimu wao Simba.

"Ni kweli wachezaji hao walimaliza mikataba yao na bado hatukuwahi kufanya nao mazungumzo, lakini baada ya kuona mahasimu wetu Simba wanawawinda tumeamua kujihami mapema," alisema.

Sendeu pia alisema suala la timu yake kucheza na mabingwa wa Carling Cup Birmingham ya Uingereza, lipo mikononi mwa Kocha Mkuu, Sam Timbe baada ya kurudi nchini Juni 12 mwaka huu akitokea kwao Uganda mapumzikoni.

Alisema hadi sasa hawajapata taarifa zozote kutoka kwa Simba, kama watatakiwa kucheza mechi hiyo, hivyo wao kama viongozi suala hilo wanamwachia kocha wao.

Birmingham inatarajiwa kutua nchini Julai 5 mwaka huu, ambapo wataanza kwa kucheza na Simba na Julai 12 watacheza na Yanga.

No comments:

Post a Comment