Na Rashid Mkwinda
SERIKALI imesema itawanyanganye leseni wafanyabiashara watakaokiuka utaratibu wa uuzaji wa mahindi yaliyoingizwa sokoni na serikali ili kudhibiti bei yake
nchini.
Akizungumza na wafanyabiashara wa mazao ya mahindi jijini Dar es salaam mwishoni mwa wiki Waziri wa Kilimo, Chakula na Mifugo, Prof. Jumanne Maghembe alisema kuwa utaratibu wa ununuzi na uuzaji ndio njia pekee itakayosaidia serikali kudhibiti uuzaji holela wa chakula nchini.
Aidha aliwataka wafanyabiashara hao kutoka Manispaa tatu za Temeke, Ilala na Kinondoni kutohifadhi mahindi hayo ili kutegea kupanda kwa bei kwa kuwa yatawadodea kutokana na kuanza kwa msimu mpya wa mavuno.
Prof. Maghembe alisema kuwa serikali imepanga kudhibiti uuzaji holela wa chakula na kuwa kila mkoa una mgawo wake wa chakula, hivyo wafanyabiashara wanatakiwa kuchukua kibali cha kununua mahindi katika eneo husika na kuuzia katika eneo analoishi ili serikali iweze kuratibu vyema chakula kutoka Hifadhi ya Taifa ya Chakula.
Kwa upande wao wafanyabiashara hao wameiomba serikali kuongeza bei ya unga wa mahindi kwa kilo moja kutoka sh. 500 hadi sh. 650 ili kufidia gharama za usafirishaji.
Walisema ili bei ya kuuza unga iwiane na bei ya kununulia mahindi serikali inatakiwa kuuza mahindi kwa sh.300 kwa kilo moja badala ya sh. 490 ambapo muuzaji anatakiwa kuuza unga kwa sh. 500.
Mfanyabiashara wa Manzese, Manispaa ya Kinondoni, Bw. Noha Chipala alisema kuwa kilo 100 za mahindi zinatoka kilo 65 za unga na hivyo kupoteza kilo 35, hivyo kitendo cha kutaka kuuzwa kwa unga sh. 500 kwa kilo ni sawa na kuwazuia wafanyabiashara hao kuwauzia unga wananchi.
Alisema kuwa tangu serikali itangaze bei yake wafanyabishara wengi wanashindwa kukoboa na kusaga mahindi waliyonunua huku baadhi yao wakidaiwa mikopo ambayo wanashindwa kuirudisha kutokana na kushindwa kuuza.
Naye Bw. Jonathan Gabone mfanyabiashara wa kutoka Temeke alisema kuwa tathmini ilizofanywa na wataalamu kutoka wizara ya kilimo haikuwashirikisha wafanyabiashara kwa kuwa kuna hatua nyingi zinazopaswa kufuatwa tangu ununuzi wa mahindi hadi kumfikia mlaji.
Akijibu maombi ya wafanyabiashara hao, Prof. Maghembe alisema kuwa serikali ilipanga bei yake ya kuuza mahindi sh. 380 kwa kilo moja, kusafirisha, kupakua, kukoboa, kusaga na upotevu na kupata jumla ya sh. 426 ambapo mkulima angepata faida ya sh. 80.
No comments:
Post a Comment