Na Addolph Bruno
WASANII wa muziki wa nchini wameitaka serikali kuufanyia mabadiliko uongozi wa Chama cha Hatimiliki Tanzania (COSOTA), baada ya kuonekana kushindwa kuwasaidia
kudhibiti uvunjifu wa sheria ya hatimiliki ya kazi zao.
Wito huo ulitolewa Dar es Salaam jana na wasanii mbalimbali wa muziki nchini walipokuwa wakiwasilisha kero zao kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo Dkt. Emmanueli Nchimbi na viongozi mbalimbali wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
Akizungumza katika mkutano huo, mmoja wa wasanii hao ambaye pia aliwahi kuwa Katibu wa Chama Cha Muziki wa Dansi Tanzania, Francis Kaswahili alisema sheria iliyowekwa kuhusu hatimiliki kwa kazi za wasanii ni nzuri, isipokuwa COSOTA ni kikwazo ambayo inaonekana kushindwa kudhibiti wizi unaoendelea kufanywa.
"Mheshimiwa Waziri, mimi ni mwanamuziki na ninaifahamu mno sanaa hii na ninakuhakikishia sheria yetu ni nzuri zaidi ya Nigeria, Ghana, Kenya na hata Uganda tatizo ni utendaji mbovu uliopo wa viongozi wetu na kama inawezekana tunaiomba serikali itupatie sisi wenyewe muone," alisema.
Naye mwanamuziki mkongwe, Cosmas Chidumule alisema tatizo jingine ni kuwepo kwa tofauti kati ya sheria ya hatimiliki Tanzania Bara na Zanzibar na kuiomba serikali kufanya marekebisho ya sheria na muundo, kwani kwa kufanya hivyo italiwezesha taifa kuingiza pesa nyingi.
Mwanamuziki Luiza Mbutu, alisema wasanii wanashindwa kuendelea kutokana na BASATA kuwakata zaidi ya sh. milioni 1.5, kabla ya kuingiza albamu sokoni huku wakiwa wamelipia sh. 200 kwa kila kopi kwa wasambazaji wao ambao na kuishauri serikali kuunda chombo maalumu kitakachosimamia mauzo yao waweze kuokoa fedha nyingi zinazopotelea mikononi mwa watu.
Akifafanua kwa ufupi kuhusu hoja hizo, Waziri Nchimbi alisema awali alikutana na Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Cyril Chami, ambako COSOTA ipo chini ya wizara hiyo kujadili maendeleo ya muziki nchini, waliona ipo haja ya kufanya mazungumzo na wasanii kusikiliza kero zao kwanza na kuahidi kuzifanyia kazi kabla ya kukutana nao tena mwishoni mwa mwaka huu.
"Niseme tu kwamba maoni yenu tumeyapokea na nakubaliana na nyinyi kwa asilimia nyingi kuhusu suala la elimu, lakini kabla ya hapo tutafanya mazungumzo na chama cha wamiliki wa vyombo vya habari, kuweka utaratibu maalumu wa jinsi gani tutaweza kuwainua na pia BASATA iratibu mashindano na vigezo vya msingi ambavyo vitawezesha kuwatangaza nyinyi kwanza," alisema.
No comments:
Post a Comment