18 May 2011

Simba yamkabidhi Basena 'rungu'

*Athuman Idd aanza mazoezi

Na Elizabeth Mayemba

UONGOZI wa Simba umemkabidhi 'rungu' Kocha Mkuu wa timu hiyo, Moses Basena kuwapitisha wachezaji anaowataka kwa ajili ya msimu ujao wa
Ligi Kuu Bara.

Wachezaji wanaotaka kusajiliwa na Simba kwa msimu ujao ni Patrick Mafisango (Azam), Nassoro Said 'Cholo' (JKT Oljoro), Athumani Idd 'Chuji' (Yanga), Salum Machaku (Mtibwa Sugar), Mwinyi Kazimoto (JKT Ruvu), Shomari Kapombe, Haruna Moshi, Ulimboka Mwakingwe (Majimaji) na Mkenya Willis Ochieng.

Tayari kikosi cha Simba, kimeanza mazoezi juzi katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya waydad de Casablanca ya Morocco.

Akizungumza Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Godfrey Nyange 'Kaburu' alisema wachezaji walioanza mazoezi ni wale wa zamani ila wapya ni Athuman Idd 'Chuji' ambaye jana jioni alifanya mazoezi na wenzake pamoja na Mnigeria Samwel Temmy na Isihaka Rajabu wa Abajalo ya Kinondoni.

Pia katika mazoezi ya jana waliongezeka Mussa Hassan 'Mgosi' na Hilary Echesa, ambao juzi hawakuwepo.

"Kazi ya kuwafanyia majaribio wachezaji wetu wapya tumempa kocha wetu Basena, akiridhishwa na viwango vya wachezaji hao, dirisha la usajili litakapofunguliwa tutaingia nao mikataba," alisema Kaburu.

Alisema pia wana nafasi mbili za kusajili wachezaji wa kimataifa, ambao wataungana na Emmanuel Okwi, Jerry Santo na Patrick Mafisango.

Kaburu alisema kwa sasa kocha huo, anaelekeza nguvu katika mchezo wao na Wydad itakayochezwa kati ya Mei 27, 28 na 29 mwaka huu, kwenye uwanja huru utakaotangazwa baadaye.

Ameongeza kuwa tayari wachezaji wao wa kimataifa Jerry Santo na Patrick Ochan, ambaye msimu ujao ataichezea timu ya TP Mazembe ya Congo, wameshajiunga na wenzao kwa ajili ya maandalizi ya michuano hiyo.

1 comment:

  1. Chonde chonde,angalieni,msichezeshe wachezaji wapya kama TP mazembe,Kumbukeni hilo,Uwakika wa kuwatoa waarabu hao upo,Kama ilivyokuwa kwa Zamaleck.Simba oyeeeeeeeee.........

    ReplyDelete