Na Addolph Bruno
CHAMA cha Michezo ya Jadi Tanzania (CHAMIJATA), kimepata mwaliko kwenda nchini China kushiriki tamasha la kimataifa la michezo hiyo yanayofahamika
kama, Qinghai International Traditional Archery Competition.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa CHAMIJATA, Mohamed Kazingumbe alisema tamasha hilo la tatu tangu kuanzishwa litafanyika katika mji wa Le Du', uliopo katika jimbo la Qinghai nchini humo kuanzia Juni 13 hadi 16 mwaka huu.
Alisema mwaliko huo umetokana na Tanzania kufanya vyema mara nyingi katika mashindano ya Duani, yanayofanyika kila mwaka nchini Korea Kusini.
"Tunapokwenda Korea mara nyingi, wachezaji wetu wanaonesha uwezo mkubwa katika michezo ya mitupo, bao, mieleka, kukuna nazi na mingine mingi hivyo kutokana na hilo wameona umuhimu wetu sisi na tumepata mwaliko huo ambao ni nafasi nyingine kwetu kuonesha uwezo wetu," alisema Kazingumbe.
Kazingumbe alisema mashindano hayo yatatanguliwa na semina elekezi itakayoshirikisha washiriki kutoka nchi 40.
Alisema katika tamasha hilo, Tanzania imealikwa kwa ajili ya mchezo mmoja kati ya nane inayochezwa na CHAMIJATA, ambao ni kulenga shabaha kwa kutumia mishale na pinde za asili ambapo wamepewa nafasi ya kupeleka wachezaji wawili.
Mwenyekiti huyo alisema wachezaji watakaokwenda katika tamasha hilo ni bingwa wa taifa mara mbili kwa upande wa wanawake mwaka 2008/2009, Kilabu Nada na bingwa kwa upande wa wanaume Maduhu Mahiya.
Alisema licha ya kukabiliwa na hali ngumu ya fedha, chama chake kipo katika harakati za kuwaandaa wachezaji hao na kuwaomba wadau pamoja na taasisi mbalimbali kuwasaidia.
No comments:
Post a Comment