01 May 2011

Uganda yaizima Vijana Stars Dar

*Watanzania watoka kichwa chini

Na Elizabeth Mayemba

TIMU ya soka ya Tanzania chini ya miaka 23 jana imeaga katika michuano ya kuwania kufuzu mashindano ya Mataifa ya Afrika, yatakayofanyika
Msumbiji baada ya kufungwa mabao 3-1 dhidi ya Uganda kwenye Uwanja Taifa, Dar es Salaam.

Uganda iliyomaliza mechi hiyo ikiwa na wachezaji 10 imesonga mbele kwa uwiano wa magoli 5-2, baada ya awali kushinda mabao 2-1 mjini Kampala, Uganda na katika hatua inayofuata itachuna na mshindi kati ya Kenya na Eritrea itakayochezwa leo Nairobi, Kenya.

Waganda wakicheza kwa lengo la kulinda ushindi wao wa awali, walianza pambano kwa nguvu na kupata penalti sekunde ya 30, ambayo ilipigwa na mchezaji wa Simba, Emmanuel Okwi na kuokolewa na kipa Shaban Kado.

Penalti hiyo ilitolewa na mwamuzi, baada ya Kado kumwangusha nchezaji wa Uganda katika eneo la hatari.

Vijana waliliongeza mashambulizi kutaka kupata goli ambapo dakika ya 10, Mbwana Samata alikosa goli.

Uganda nayo iliongeza mashambulizi ya nguvu na kupata goli la kwanza dakika ya 17 kupitia kwa Sadam Ibrahim ambaye alipiga shuti liligonga mwamba wa juu na mpira kudunda chini ambapo Kado katika harakati za kuokoa aliusindikiza wavuni kwa mgongo.

Bao la pili la Uganda, liliwekwa kimiani na Hamis Kizza dakika ya 34 baada ya kupokea pasi ya Michael Mutyaba.

Dakika ya 27 Vijana Stars ilikosa goli baada ya Juma Abdul, kumkatia pande zuri Thomas Ulimwengu aliyepiga mpira pembeni ya goli.

Dakika ya 37, mchezaji Ivan Bukenya wa Uganda alioneshwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kipepsi Ulimwengu.

Vijana Stars ilipata uhai kipindi cha pili baada ya Samatta, kufunga goli dakika 56 kwa kupiga mkwaju akiwa wingi ya kushoto iliyokwenda moja kwa moja kimiani.

Samatta ambaye jana alikuwa na ulinzi mkali angekuwa makini angeweza kufunga bao jingine dakika tatu baadaye na kisha Ulimwengu naye alikosa goli dakika 61.

Jitihada za vijana hao wa Tanzania kupata bao la kusawazisha zilififia, baada ya Ugenda kufunga bao la tatu dakika ya 82 kupikia kwa Kizza akiunganisha mpira wa kona ya Owen Hasule.

Vijana Stars jana licha ya Uganda kuwa pungufu lakini, ilishindwa kabisa kujipanga kupata mabao baada ya kujikuta wakilinda lango badala ya kushambulia.

No comments:

Post a Comment