01 May 2011

Taifa Stars kuingia kambini kesho

Na Addolph Bruno

TIMU ya taifa 'Taifa Stars' inaingia kambini kesho kujiandaa na mechi ya marudianao dhidi ya Afrika ya Kati  itakayochezwa Juni 4, mwaka huu nchini humo.Mechi hiyo ya
kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika ni marudiano baada ya awali Taifa Stars kushinda mabao 2-1 iliyofanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema kikosi kitakachoingia kambini ni kile kilichocheza mechi ya kirafiki Jumamosi iliyopita dhidi ya Msumbiji mjini Maputo.

"Timu haitakuwa na mabadiliko, wachezaji watakaoingia kambini watakuwa ni wale wale waliocheza na Msumbiji na tunaanza kambi mapema ili kuhaikisha timu inafanya vizuri katika mchezo huo," alisema.

Katika mchezo dhidi ya Msumbiji ambao ulikuwa maalumu kwa ajili ya sherehe za  ufunguzi wa uwanja wa kisasa wa nchi hiyo, Stars ilifungwa mabao 2-0.

Wakati huo huo, Wambura alisema bado wanaendelea kufuatilia ujio wa timu ya Taifa ya Afrika Kusini 'Bafana Bafana', ambayo itacheza na Stars mechi ya kirafiki Jijini Dar es Salaam.

Alisema mpango huo unaendelea na ukikamilika shirikisho hilo litatoa taarifa mapema, ili kuwafahamisha mashabiki wa soka kuhusu mechi hiyo ambayo ni muhimu kwa Stars, kujiandaa kabla ya kuikabili Afrika ya Kati.

No comments:

Post a Comment