19 May 2011

Timu ya mpira wa meza kucheza Zambia

Na Mwali Ibrahim

TIMU ya taifa ya mpira wa meza, imepata mwaliko wa kushiriki katika mashindano ya kimataifa ya Four National Championship yanayotarajia kufanyika
Julai 26 mwaka huu, Zambia.

Katika mashindano hayo Tanzania itakuwa inatetea taji hilo ambalo ililinyakua mwaka jana nchini Zambia.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ramadhan Othman alisema mashindano hayo yatashirikisha nchi za Tanzania, Malawi, Zimbabwe na wenyeji Zambia.

Alisema mashindano hayo yatawasaidia kuwaweka fiti wachezaji wake ambao wanakabiliwa na mashindano mengine yatakayofanyika nchini Zimbabwe ambayo yatashirikisha nchi tisa.

Alizitaja nchi watakazochuana nazo katika mashindano hayo ya Zimbabwe Julai mwaka huu kuwa ni Zambia, Msumbiji, Malawi, Afrika Kusini, Kenya, Uganda,  Zambia, Tanzania na wenyeji Zimbabwe.

Alisema, mashindano hayo ni kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Mataifa ya Afrika yatakayofanyika Septemba mwaka huu nchini Msumbiji.

Othman alisema, timu inaendelea na mazoezi katika Ukumbi wa Shule ya Kisutu kwa ajili ya kujiandaa na mashindano hayo.

No comments:

Post a Comment