LONDON, Uingereza
MABINGWA wa Kombe la FA, Manchester City usiku wa kuamkia leo wameifunga Stoke City kwa mara ya pili katika muda wa siku nne na kupanda hadi nafasi ya
tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
Hatima ya nahodha na mshambuliaji wa City, Carlos Tevez bado iko kwenye hati hati lakini aling'ara katika mechi hiyo kwa kufunga mabao mawili na kuipa ushindi wa mabao 3-0 uliopatikana katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Eastlands.
Mabao yake mawili yamefanya awe sawa kwa idadi ya mabao na Dimitar Berbatov, ambapo kila mmoja ana mabao 20.
Mchezaji huyo wa Argentina, alifunga kwa jitihada zake binafsi kwa kupiga shuti katika dakika ya 14.
Joleon Lescott alifunga bao jingine dakika 53 na kisha Tevez, alifunga tena dakika ya 65 na kuifanya City kupata ushindi wa mabao 3-0 ambao uliipandisha nafasi ya tatu na kufikisha pointi 68 wakiizidi Arsenal, pointi moja huku ikiwa imebakiwa na mechi moja.
Manchester United ambayo tayari imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, iko nafasi ya kwanza, ina pointi 77 ikifuatiwa na Chelsea ambao ni mabingwa wa msimu uliopita wenye pointi 71,
Kama itaweza kumaliza Ligi ikiwa katika nafasi hiyo, City itacheza Ligi ya Mabingwa kwa kuingia moja kwa moja katika hatua ya makundi.
Stoke, waliingia katika mechi hiyo huku wakionekana kuchoka, pengine ni kutokana na kucheza fainalia ya FA dhidi ya City, inayonolewa na kocha Roberto Mancini Jumamosi.
City ilicheza vizuri huku wachezaji Tevez, James Milner na Yaya Toure wakikosa magoli katika dakika za mwanzo kabla ya kufunga magoli na kuongoza dakika dakika 15 za mwanzo.
Tevez alifunga goli la kwanza kwa kupiga chenga mabaki wawili na kupasiana na Milner, kisha aliwapiga chenga wengine wawili na kufunga katika umbali wa yadi 15.
Micah Richards na Milner nao walikosa nafasi nzuri za kufunga.
Stoke nayo ilipata nafasi dakika ya 35 kupitia kwa Glenn Whelan, lakini shuti lake lilipanguliwa na Joe Hart.
No comments:
Post a Comment