Na Zahoro Mlanzi
UONGOZI wa Klabu ya Simba, umeamua kuipeleka timu yake Zanzibar kwa ajili ya kupiga kambi ya wiki moja leo, Zanzibar kabla ya kucheza na wapinzani na
Wydad Casablanca ya Morocco katika mechi ya Klabu Bingwa Afrika.
Mchezo huo ambao ni wa kuwania kutinga hatua ya makundi utapigwa kwa mkondo mmoja, umepangwa kupigwa Mei 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Petrosport jijini Cairo, Misri
Simba ilipata nafasi hiyo ya kuwania kutinga hatua hiyo baada ya waliokuwa mabingwa watetezi, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kuondolewa mashindanoni kutokana na kumchezesha mchezaji kinyume na taratibu.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Rage alisema wanachama wa Simba waliopo Zanzibar wameiomba timu hiyo ikapige kambi huko ili nao watoe mchango wao.
"Unajua sasa hivi Simba ndiyo timu pekee inayoiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa, hivyo kwa kuheshimu suala la Muungano wetu na Zanzibar, ndiyo maana tumeamua timu hiyo ikapige kambi huko," alisema Rage.
"Wanachama wetu wa Zanzibar, walituomba wapate nafasi ya kuwafunda wachezaji wetu kabla hatujacheza na Wydad Casablanca, hivyo tumeheshimu maombi yao na timu kesho (leo) itakwenda Zanzibar," alisema.
Alisema wana imani kwa muda watakaokuwa Zanzibar, timu yake itafanya maandalizi mazuri ya kuhakikisha wanavuka hatua hiyo ya tatu ya michuano hiyo na kutinga nane bora.
Akizungumzia suala la Mbwana Samatta, ambaye wamemuuza hivi karibuni kwa TP Mazembe, alisema wameshazungumza na timu hiyo kuhusu kumruhusu mchezaji huyo kuja kuisaidia wakati watakapocheza na Wydad Casablanca.
Alisema kwa mujibu wa sheria wana uwezo wa kumtumia mchezaji huyo pamoja na Patrick Ochan, ambaye naye aliuzwa huko lakini wameliandikia barua Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), ili kupata muongozo wa suala hilo.
"Najua kisheria tunaweza kuwatumia Samatta na Ochan kwani ITC (Hati ya Uhamisho wa Kimataifa) shirikisho letu (TFF), halijatoa lakini ni vizuri tukawashirikisha CAF katika hili mapema, ili tujue watasemaje maana tunaogopa lisije likatokea la kutokea huko mbele," alisema Rage.
Timu hiyo iliingia kambini kujiandaa na mchezo pamoja na michuano ya Kombe la Kagame Jumatatu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo wachezaji wapya na wazamani walianza mazoezi hayo yaliyo chini ya Kocha MKuu, Mosses Basena.
Baadhi ya wachezaji walioanza mazoezi ya pamoja ni makipa Juma Kaseja na Ally Mustapha 'Barthez', Juma Jabu, Jerry Santo, Kelvin Yondani, Hilary Echessa, Nicco Nyagawa, Haruna Shamte na Amri Kiemba.
Wengine ni Juma Nyosso, Ali Ahmed 'Shiboli', Abdulhalim Humud, Aziz Gila, Shija Mkina, Uhuru Selemani, Amir Maftah na Samwel Temi anayetoka nje ya nchi.
No comments:
Post a Comment