01 May 2011

Timbe akaribisha 'Maproo' Yanga

Na Elizabeth Mayemba

KOCHA Mkuu wa Yanga, Sam Timbe amesema hatafukuza wachezaji wa kimataifa ambao wanataka kuja kufanyiwa majaribio, wakati timu yake itakapoanza
rasmi mazoezi.

Tayari wachezaji mbalimbli kutoka Afrika Magharibi, wameanza kumiminika katika kikosi hicho kwa ajili ya kuomba kufanyiwa majaribio.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana kwa simu akiwa Uganda, Timbe amewataka viongozi wa klabu hiyo, wawaache wachezaji wanaotaka kufanyiwa majaribio, kwani huenda kukawa na wachezaji wazuri zaidi, pamoja na kwamba nafasi za wachezaji wa kigeni za kusajiliwa ni finyu.

"Nawakaribisha wote wanaotaka kufanya majaribio na kikosi changu, waje tu pindi tutakapoanza mazoezi rasmi kwani hiyo pia itakuwa ni changamoto kwa wachezaji wangu, wanaweza kuambulia mbinu mpya," alisema Timbe.

Alisema hata yeye mwenyewe amekuwa akipitia mtandao na kuona maombi mbalimbali ya wachezaji wa kigeni, ambao wanataka kufanyiwa majaribio kwa lengo la kusajiliwa.

Timbe alisema anaamini msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa, atakuwa na kikosi bora ambacho kitakuwa tishio kwa Afrika Mashariki.

Wachezaji kutoka nchi za Ivory Coast, Cameroon, Zambia, Nigeria na Ghana wameomba kujaribiwa na klabu hiyo yenye masikani yake mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment