20 May 2011

Tibaijuka: NHC dai kodi hata serikalini

Na Anneth Kagenda

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Anna Tibaijuka amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuhakikisha inadai kodi bila kuacha mteja
yeyote, hata kama taasisi za serikali.

Hayo aliyasema Dar es Salaam jana wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika, chenye lengo la kujadili masuala ya utendaji yanayolenga kuongeza tija kwa shirika na kupitia bajeti yake ya mwaka 2011/2012.

Vile vile alilitaka shirika hilo kuongeza idadi ya nyumba, akisema, "NHC ndiyo imepewa dhamana na serikali ya kuongoza mageuzi ya nyumba hapa nchini, hivyo mnayo changamoto kubwa ya kupanua shughuli za ujenzi ili kupunguza uhaba wa nyumba uliopo ambao unakaribia kufikia milioni tatu.

Alisema kuwa anaelewa kuwa hivi sasa shirika hilo linakusanya kodi na malimbikizo kutoka kwa watu binafsi na taasisi za serikali, na kuongeza kuwa hawana budi kuendelea na moto huo huo kwani kodi ndizo zinazowezesha kutoa huduma bora zaidi na kutekeleza mipango mingine iliyopangwa.

"Hatuwezi kuendelea kuvumilia watu wachache wenye ubinafsi wa kutolipa kodi ambayo ina manufaa makubwa kwa Watanzania wote, hivyo naziasa Wizara na Taasisi za Serikali kuhakikisha kuwa zinalipa kodi kwa wakati kwa kuwa zinatengewa fedha hizo katika bajeti zao," alisema.

Waziri Tibaijuka alisema kuwa hivi sasa wizara yake haipelekewi malalamiko mengi yanayohusu NHC na kusema kuwa anawaomba kuendelea na juhudi hizo za kujenga taswira yao ili hatimaye chombo hicho kiweze kukidhi matarajio ya Watanzania.

Alisema wizara yake imeanza kuyafanyia kazi masuala yote waliyoainisha ili kuliwezesha shirika hilo kuwa na nguvu za kusimama na kuendeleza makazi nchini.

"Ndio maana serikali imeunda chombo cha kutoa mikopo ya nyumba kwa mabenki ili nayo yaweze kutoa mikopo ya muda mrefu na riba nafuu kwa wajenzi na wanunuzi wa nyumba na kusema kuwa hizo zote ni juhudi za serikali za kuwezesha sekta ya nyumba kuwa endelevu," alisema.

Kuhusu gharama za nyumba, alisema, "Napenda kusisiza kuwa jengeni nyumba za kuwawezesha watu wa kipato cha chini na kati kuzinunua kwani benki nyingi haziwezi kuwapa watu wengi mikopo mikubwa mikubwa, na pia serikali ingependa kuona Watanzania wengi wananufaika na mipango mizuri ya shirika hilo," alisema Waziri Tibaijuka.

2 comments:

  1. Heko mama Prof. huu ndiyo uwajibikaji kaza uzi uokowe wanyonge, mtanzania wa kawaida ananunua haki nchini kwake. Tunataka mtu jasiri siyo hao wanao nunuliwa kirahisi rahisi kuwaacha wengi Raia wakiteseka. Mungu Akulinde

    ReplyDelete
  2. TUNAWATU TUNAWAJUA KUWA KAMA WANGEKUWA KWENYE MFUMO MZURI WA UTAWALA WANGEFANYA ZAIDI YA HAYO WANAYOYAFANYA.ILA SASA TATIZO NI SISI MINYAWATU, HAWATAKI KUKOSOLEWA HATA KUSHAURIWA MBELE YA KADAMNASI WAO WANAJIONA MIUNGU WATU.
    PROF. AKISHAURI ANAWEZA HATA AKAONEKANA MPINZANI JINSI SISI MINYAWATU WALIVYO NA VISA

    ReplyDelete