20 May 2011

CHADEMA yatuma wanasheria waliouawa Tarime

Na Tumaini Makene

CHAMA cha Demokrasia kimeingilia kati suala la mauji ya raia yaliyofanywa na Jeshi la Polisi, huko Tarime, kwa kupeleka wanasheria wake wilayani humo, kufuatilia kwa kina
kilichojiri kisha kuwasaidia wafiwa kupata haki, huku pia kikitoa tamko kumtaka Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, balozi Khamis Kagasheki, asiume maneno kusema ukweli juu ya maafa hayo.

Akitoa tamko hilo Mjini Iringa jana, Mwenyekiti wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe alisema kuwa chama hicho, kinataka kuundwa kwa Tume ya Kisheria ya Majaji wa Mahakama Kuu, kuchunguza kwa makini jumla ya vifo vya Watanzania 20 waliokwisha kuuawa tangu mwaka 2006, katika Mgodi wa North Mara unaomilikiwa na Kampuni ya Barrick ili ukweli ujulikane.

Alidai kuwa kwa mujibu wa uchunguzi wao CHADEMA, watu hao waliouawa juzi walipigwa risasi kwa nyuma, si kwa mbele, hali ambayo ingeweza kuonesha kuwa walikuwa wakipambana na askari polisi, hivyo hakitakubali kuona marehemu hao wakizikwa haraka haraka bila miili hiyo kufanyiwa uchunguzi wa kina na Jeshi la Polisi kutoa tamko juu ya mauaji hayo.

"Napenda kutumia fursa hii kutoa tamko juu ya mauaji ya raia yaliyofanywa na askari polisi huko Tarime, naomba Watanzania mnisikilize kwa makini sana...mgodi wa North Mara ulioko Nyamongo unamilikia na Barrick...juzi polisi wamewapiga risasi raia...taarifa zilizopo zinasema waliouawa ni watano, lakini taarifa zetu zinaonesha waliouwawa wako tisa.

"Mpaka sasa polisi hawajasema lolote juu ya mauaji hayo...jana Waziri wa Mambo ya Ndani Kagasheki kasema kuwa kuna chama kinawachochea watu wa Tarime wafanye maandamano na mikutano, tunamtaka asiume ume maneno, chama kilichokuwa kimeomba kufanya maandamano na mikutano Tarime ni CHADEMA...siku zote serikali imekuwa ikisimama upande wa wawekezaji hao na kuwaacha raia.

"Tangu mwaka 2006 mpaka hiyo juzi wameuawa watu 20, lakini hakuna uchguzi wowote wa kina umewahi kufanywa juu ya mauaji ya raia huko Tarime...sasa sisi tunasema kuwa tutawasaidia wafiwa hao...tumeshamtuma Mbunge wa Arusha Mjini, Lema na Mbunge wa Viti Maalum Tarime, Easter, kuwasaidia ndugu kupata haki," alisema Bw. Mbowe na kuongeza;

"Kesho wanasheria wetu wakiongozwa na Marando (Mabere) na Tundu Lissu wanakwenda Tarime, kisha viongozi wakuu tunafuata huko...tunasikia polisi wanawadanganya wananchi wazike bila miili hiyo kufanyiwa uchunguzi...sasa tunasema ngoma inatoka Nyanda za Juu Kusini inakwenda Tarime mpaka kieleweke. Hakuna raia ambaye hana haki ya kuishi hata kama ni mwizi au jambazi.

"Taarifa zinasema kuwa hakuna marehemu hata mmoja katika hao waliouwa ambaye amepigwa risasi kwa mbele, wamepigwa risasi kwa nyuma...tunamtaka waziri asiume maneno...Chadema kitafanya maandamano na mikutano mpaka kieleweke...wangeweza kuwapiga risasi za miguuni kisha wafikishwe kwenye vyombo vya sheria...hatutetei wezi lakini hatukubali raia kuuwawa."    

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibrod akihutubia maelfu ya wakazi wa Iringa katika Viwanja vya Mlandege, alisema kuwa Tanzania Serikali ya Tanzania haistahili kupokea fedha za fidia kutoka Kampuni ya BAE System ya Uingereza katika ununuzi wa rada, akisema "ni bora fedha hizo zikaenda kwa NGO ilimradi tu kuwe na uhakika na uhalali wake.

"Bora zipitie katika NGO halali kuliko hizo fedha kupitia kwa serikali ya kifisadi...namwambia Membe kuwa serikali yake anayosema ni huru ilishapoteza uhalali wa kupata fedha hizo tangu iliposhindwa kuchunguza ufisadi wa rada...waliambiwa na SFO kuwa kuna fedha za rada zimewekwa Uswisi kisha zikahamishiwa Uingereza huko New Jersey.

"Wakaambiwa wachunguze akaunti hiyo ya Chenge na mke wake huko Uingereza, serikali yetu ambayo Membe anasema kuwa ni huru, ikashindwa kuchunguza ikisema kuwa inasubiri Uingereza kwa kutumia sheria zake ndiyo ifanye uchunguzi...sasa uhuru wetu ambao kweli tunao, uko wapi hapo," alisema Dkt. Slaa.

2 comments:

  1. CHADEMA WANAJITAHIDI SANA, JAPO TUNAJUA KUWA KWA KATIBA HII HAKI ZINAPINDISHWAPINDISHWA MUONE WENZENU WALIVYO SIRIAZI. YULE JAMAA ALIYETAKA KUBAKA WA IMF JAPO ANACHEO KIKUBWA DUNIANI LAKINI ALIKAMATWA NA KUWEKWA NDANI.

    TANZANIA!!!UKIWA NA MAHUSIANO MAZURI NA MTU FULANI BASI UTAISHI JUU YA SHERIA.

    ReplyDelete
  2. Toka lin jambaz anapewa rambirambi na serikal..hapa kuna kitu..jaman polis mbona mnatumaliza ndo mana raia wanawaua na nyie..MNAZIDI KUONGEZA CHUKI KWA RAIA NA SERIKAL YAKE

    ReplyDelete