18 May 2011

DC kuwasaka wanaorusha sukari

Na Edgar Nazar, Bagamoyo

MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo, Bw. Mugesa Mulongo ametangaza vita na wafanyabishara ambao bado wanakaidi agizo la Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda la
kushusha bei ya sukari na kuwa sh. 1,700 ili kumnusuru Mtanzania wa kawaida kutokana na kupanda kwa bidhaa hiyo kiholela.

Kauli hiyo aliitoa jana wakati akifunga kikao cha Ushauri wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo (DCC) kilichofanyika kwenye ukumbi wa chuo cha Uongozi wa Ualimu (ADEM) mjini hapa.

“Napenda niwatahadharishe wafanyabishara kwamba natangaza vita na nitapita huko kwenye maduka na kama nitamgundua mfanyabiashara ambaye bado anauza sukari bei juu tutamnyang'anya leseni ya kufanya biashara na na tutamtangaza ili asiweze kupata leseni sehemu nyingine nchini,” alisema mkuu huyo wa wilaya.

Alisema kuwa tayari ameshawasiliana na maafisa wa kitengo cha biashara wa wilaya ambao watatekeleza hilo haraka ili kuwanusuru wakazi wa wilayani hapa ambao wanalalama kila kukicha kuwa sukari bado inauzwa bei juu licha kuwa inapatikana kwa wingi tofauti na hapo nyuma.

Mkuu huyo wa wilaya ambaye alionesha kukerwa na ukaidi wa agizo hilo, amedai kuwa wafanyabishara wakubwa anajua kuwa wananunua sukari Zanzibar na anashangaa bado kuona kuwa inakuwa bei juu licha ya kuwa wanaipata kwa bei chee.

Hivyo alisema kuwa zoezi la ukaguzi kupitia duka hadi jingine atashirikiana na mmaofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kufanikisha malengo kuanzia Bagamoyo na baadaye kuhamia Chalinze ambako sukari inauzwa mpaka sh 2,300 kwa kilo moja.

No comments:

Post a Comment