19 May 2011

Simba, Wydad kukipiga Cairo

Na Zahoro Mlanzi

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF), limeamua mchezo wa mkondo mmoja uliopangwa upigwe uwanja huru, kati Simba na Wydad Casablanca ya
Morocco utapigwa Mei 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Petrosport Jijini Cairo, Misri.

Simba imepata nafasi hiyo ya kuwania kutinga hatua ya makundi baada ya waliokuwa mabingwa watetezi, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kuondolewa mashindanoni kutokana na kuchezesha mchezaji kinyume na taratibu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alieleza kuwa iwapo muda wa kawaida wa dakika 90 utamalizika kwa sare, mshindi atapatikana kwa mikwaju ya penalti.

"Wenyeji wa mechi (kwa maana watakaohusika na kupokea timu na viongozi uwanja wa ndege) na gharama zingine za mechi hiyo, zitabebwa na timu husika na Chama cha Mpira wa Miguu cha Misri (EFA)," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Wambura alisema kila timu itajigharamia usafiri wa kwenda Cairo, pamoja na gharama za malazi na kwamba EFA imeombwa kusaidia timu zote katika maandalizi ya hoteli za kufikia.

Alisema gharama za maofisa wa mchezo (waamuzi na kamishna), ukiwemo usafiri na malazi zitabebwa na klabu hizo kupitia vyama vyao vya TFF na FRMF.

Aliongeza kwamba gharama zozote ambazo EFA, itatumia katika maandalizi ya mechi hiyo zitarejeshwa na TFF na FRMF.Pia mapato yatakayopatikana kutokana na viingilio katika mechi hiyo, EFA itayagawa nusu kwa nusu kwa klabu hizo kupitia vyama vyao vya mpira wa miguu.

No comments:

Post a Comment