Na Daud Magesa, Mwanza
MWANAFUNZI wa Shule ya Msingi Igoma, Wilaya ya Nyamagana Jijini Mwanza Mianzo John (14) ameuwa kwa kuchomwa kisu tumboni na mtu
asiyefahamika.
Marehemu ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba katika shule hiyo aliuawa Mei 23 mwaka huu majira ya saa 12:45 wakati akirejea nyumbani kwao katika kitongoji cha Busega Kata ya Buswelu Wilayani Ilemela.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusiana na tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Simon Sirro alisema marehemu alikwenda kumsamilimia dada yake ambapo njiani alikutana na kijana mmoja ambaye alimchoma kisu kwenye kitovu,kisha kutokomea kusikojulikana.
Kamanda Sirro alisema polisi walipokea taarifa ya kuchomwa kisu mwanafunzi huyo kutoka kwa dada yake Bi. Rosemary John (35) ambapo polisi walikwenda eneo la tukio kumchukua na kumkimbiza katika hospitali ya Mkoa wa Mwanza,Sekou Toure lakini akafariki njiani, na mwili wake umehifadhiwa katika hospitali ya Rufaa Bugando (BMC) kwa uchunguzi.
Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi Mwanza linamshikilia dereva wa pikipiki Bw. Musa Joseph (36) kwa tuhuma za kumgonga mwenda kwa miguu na kusababisha kifo.
Kamanda Sirro alisema tukio hilo lilitokea katika barabara ya Mwanza-Musoma, majira ya saa 2:30 asubuhi eneo la Nyakato National, wilaya ya Nyamagana mkoani hapa.
Alieleza kuwa mtuhumiwa huyo, akiendesha pikipiki isiyokuwa na namba za usajili alimgonga Bw. Abeid Ayoub (36) na kumsababishia majeraha, ambapo alifariki akipata matibabu katika Hospitali ya Rufaa Bugando (BMC) jijini Mwanza.
No comments:
Post a Comment