25 May 2011

Barrick: Tutashiriki kikamilifu kudhibiti migogoro

Na Edmund Mihale

KAMPUNI ya Uchimbaji Madini ya Barrick imesema inatarajia kushirikiana na wadau wote, ikiwa ni pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa jamii na
wafanyakazi wa kampuni hiyo ili kuepusha migogoro kabla ya kutokea.

Taarifa iliyotolewea kampuni hiyo kwa vyombo vya habari Dar es Saalam jana, ilieleza kuwa tayari Barrick imeiingia ubia na Taasisi isiyo ya Kiserikali iitwayo Search For Common Ground (SFCG) ili kutekeleza mradi wa mwaka mmoja uitwao 'Ujenzi wa Amani na Ulinzi Endelevu'

Ilieza kuwa msukumo wa mradi huo ni kipaumbele cha kampuni hiyo cha kuhusisha pande zote kwenye utekelezaji wa mafunzo kuhusu Kanuni za Hiari za Ulinzi na Haki za Binadamu kwa vyombo vya dola kwenye migodi yake minne ya North Mara, Buzwagi, Bulyanhulu na Tulawaka.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa hatima ya yote ni kwamba mradi huo utakuwa na manufaa ya muda mrefu wa kuboresha uhusiano katika jamii ya North Mara.

"Ni mategememeo yetu kuwa hatua hiyo pia itaibua mijadala ya wazi kuhusu ukweli wa vyanzo vilivyopo au ambavyo vinaweza kutokea vya migogoro ambayo nayo inaweza kuleta au imeleta matatizo katika jamii ya North Mara," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

"Tutaendelea na jitihada za mawasiliano katika ngazi zote za serikali pamoja na taasisi zake ili kutafuta suluhisho la kudumu. Ni matumaini yetu kuwa wadau wote na vyombo vya ulinzi na usalama vitapata msaada wa ziada na ushirikiano mzuri katika kazi ya kuimarisha ulinzi ili kuepusha matukio kama haya.

"Tunatambua juhudi za serikali katika kujenga mazingira bora ya uwekezaji ili kuongeza pato la nchi na hatimaye kuboresha maisha ya Mtanzania. Na ni matumaini yetu kuwa juhudi za makusudi zitafanywa ili kusisitiza umuhimu wa kuhakiki taswira ya Tanzania kama kituo bora cha uwekezaji.

Ilieza kuwa amani na utulivu mkoani Mara imekuwa tatizo la kihistoria, kwa kuwa Mgodi wa North Mara hushambuliwa mara kwa mara.

Ilieleza kuwa mgodi huo uko karibu na mpaka wa Tanzania na Kenya, na huwavutia wapita njia, wahalifu pamoja na wachimbaji haramu. Eneo hilo liko pembezoni, lenye maendeleo hafifu na miundombinu ya umma ni haba.

Ilieleza kuwa mazingira hayo ni chachu ya uvunjifu wa amani na utulivu, ikiwa ni pamoja na uhalifu sugu. Wanavijiji walio jirani na mgodi huo wanakabiliwa na changamoto za ukosefu wa ajira, umaskini na uhaba wa huduma za jamii.

No comments:

Post a Comment