25 May 2011

Makali ya mgawo uzembe wa TANESCO

Na Edmund Mihale

UZEMBE wa wanasheria wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) wa kutopitia baadhi ya vipengele katika mkataba kuuziana umeme kati yake na na kampuni ya
kuzalisha ya umeme ya Songas umesababisha makali mgawo wa umeme nchi.

Mgawo huo wa siku nane ulianza Mei 19, mwaka huu hadi kesho umetokana na kampuni hiyo kufanyia ukarabati visima vya gesi katika kisiwa cha Songosongo vyake na kusababisha upungufu wa megawati 350 kwenye gridi ya taifa.

Akizungumuza katika Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw. January Makamba alisema kuwa iwapo wanasheria wa shirika hilo wangepitia kwa makini mkataba huo wangeepusha nchi na mgawo huo.

"Katika moja ya vipengele vya mkataba huu vinaeleza kuwa iwapo itatokea hitilafu au tatizo lolote njia moja wapo itumike au zote, mafuta au gesi, sasa leo mnatuambia kuwa mgawo unatokana na kufanyia ukarabati visima vya gesi, je, kwa nini mliwaruhusu kuvifanyia ukarabati bila kupitia mkataba?" alihoji Bw. Makamba.

Alisema haridhiki na hatua zilizochukuliwa na shirika hilo kwa kuwa walikuwa na nafasi ya kuwaeleza watalamu wa Songas wakabadilisha mfumo kutoka gesi na kutumia mafuta ili kuendelea kuzalisha umeme na kupunguza makali ya mgawo.

Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Bw. William Mhando alisema katika mikutano yao na Songas walikubaliana kuwa wakati kampuni hiyo inafanya ukarabati huo pia ilitakiwa kutafuta kifaa kitakachobadili mfumo huo.

Pamoja na makubaliano ya kuweka mfumo huo, ilitakiwa kupanda kwa gharama za umeme kwa siku hizo nane hali ambayo alisema kuwa ingewaumiza wanachi.

Alisema kuwa shirika hilo lina changamoto nyingi kutokana kuzidai taasisi za serikali na watu binafsi fedha nyingi, hali inayolifanya lishindwe kukopesheka na kuwa taabani kifedha.

Hata hivyo, ufafanuzi huo haukumridhisha Bw. Makamba na kuwataka kusoma vizuri mkataba huo.

"Jamani mimi nasoma mkataba huu 'it doesn't make sense to me' (hainingii akilini) hivi unakwenda kununua gari kwa gharama kubwa kwa kuwa lina mfumo wa kutumia gesi na mafuta wakati huo huo. Kwa maana ya kuwa likiishiwa gesi unaweka mafuta na kuondoka, sasa linaharibika upande wa mafuta hivyo linatakiwa  kuingizwa gesi unasema kuwa ni gharama hii sikubaliani, kasomeni vizuri mkataba huu mimi nimesoma nimeelewa hivyo," alisema Bw. Makamba.   

Alisema kuwa mgawo umekuwa ukipoteza sh. bilioni 4 kila siku na Mamlaka ya Kodi nchini (TRA) ikitarajia kutokusanya sh. bilioni 840 kwa mwezi huku pato la taifa likitarajiwa kushuka kwa asilimia 5 ambazo ni sawa na dola za Marekani bilioni 1.8.

Alisema mgawo huo umesababisha pia viwanda kufungwa kupunguza ajira na gharama za bidhaa kupanda kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji.

1 comment:

  1. Inasikitisha kwa kweli, Tatizo si kwamba wataalamu hakuna bali ni Ubinafsi ulio kithiri na Wakupindukia na kukosa Uzalendo.Hauhitaji bachelor degree kuona uozo wetu Watanzania,Kila kukicha hali ya Mtanzania inazidi didimia mpaka leo hii tunategemea misaada kutoka kwa mashirika manyonyaji sio kwamba hatulijui hili bali ni kukosa uzalendo na gharama ya kutokuwa na huo Utanzania ni kubwa mno na kila mtazania atailipa mpaka hapo tutakapo amua kuwa WATANZANI NA WAZALENDO kwa maendeleo ya nchi yetu.
    "Mungu ibariki Tanzania"

    ReplyDelete