20 May 2011

Mke wa rais achangia shule milioni 1

Na Daud Magesa,Bunda

MWENYEKITI wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma Kikwete ametoa msaada wa sh. 1,000,000 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Shule ya
Msingi Ushahi wilayani Bunda Mkoa wa Mara.

Mama Kikwete alitoa fedha hizo jana wakati akizindua vyumba vitatu vya madarasa na ofisi ya walimu, vilivyojengwa kwa ushirikiano kati ya Twiga Portland Cement Ltd (TPC) ya Dar es Salaam na Mwanza Huduma Ltd ya Mwanza.

Akitoa msaada huo, Mama Kikwete alisema ametoa kiasi hicho kuunga mkono juhudi zilizooneshwa na kampuni hiyo ya saruji hasa Bw. Zulfikar Nanj ambaye ni aliwahi kuwa mwanafunzi wa shule hiyo.

“Namshukuru sana Bw. Nanj kwa kukumbuka kule alikotoka, ni wachache sana wanaokumbuka hilo, hivyo natoa sh milioni 1 ambazo zitasaidia kuboresha mazingira ya shule yhii,” alisema.

Naye Mbunge wa Viti Maalamu, Rosemary Kirigini aliahidi kujenga chumba kimoja kwa niaba ya wazazi wake, ambao kwa nyakati tofauti walipitia katika shule hiyo.

Alisema atajenga jengo hilo ikiwa ni ishara ya kuwaenzi babu yake, Daniel Kirigini ambaye aliwahi kufundisha katika shule hiyo na baba yake mzazi Herman Kirigini aliyewasoma katika shule hiyo.

Wengine ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Bi. Amina Nassoro Makilagi ambaye aliahidi kuchangia sh 500,000, Kaimu Mkuu  wa Mkoa wa Mara, Kapteni Mstaafu, Geofrey Ngatuni naye aliahidi kuchangia sh 500,000.

Awali, Kapteni Ngatuni, akitoa taarifa kwa Bi.Salma alisema mkoa huo unakabiliwa na changamoto za upungufu wa walimu, madawati, vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo.

Alieleza kuwa mkoa huo unahitaji walimu 2,972 wa madaraja mbalimbali ili kukidhi mahitaji yaliyopo ya walimu 9,893, ambapo sasa kuna uwiano wa wastani wa mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi 60.

Mkoa huo una upungufu wa vyumba 1,092 vya madarasa, madawati  81,528, matundu ya vyoo 10,612 na nyumba za walimu 8,575.

1 comment:

  1. Mbali na kuwa mke rasmi nambari wani wa Rais (First Lady), huyu Mama Salma Kikwete ana nafasi gani ya kiutendaji katika Serikali ya Jamhuri ya muungano ya Tanzania, na majukumu yake kiserikali ni yapi?!
    Mara nyingi napata shida sana ya kuelewa jambo hili.
    Juzi alikuja Musoma na dege la serikali (ambalo lilikaa kwa siku mili Musoma air port likimsubiri amelize ziara zake mkoani Mara)
    Kila mara hupokelewa na kusindikizwa kila aendapo kwa misafara mirefu ya magari ya serikali!

    Je, hili jambo ni sahihi?

    Hivi taifa letu la Tanzania litapata hasara gani au hathari zipi endapo huyu mama atapunguza au kuacha kabisa kufanya ziara hizi azifanyazo kwa gharama za walipa kodi wa nchi hii?

    ReplyDelete