15 May 2011

Mfanyabiashara mbaroni kwa mauaji ya 'Houseboy'

Na Grace Michael

MFANYABIASHARA Mkazi wa Kivule, Kata ya Kitunda, Dar es Salaam, Bw. Africanus Msele (45) anashikiliwa na Polisi Mkoa wa Ilala kwa tuhuma za mauaji ya
mfanyakazi wake wa ndani.

Akizungumza na Majira kwa njia ya simu, Kamanda wa Mkoa wa Ilala, Faustine Shilohile alithibitisha kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo juzi baada ya kutuhumiwa kufanya tukio hilo lakini akasema kuwa kutokana na utata wa kifo hicho, jeshi linasubiri taarifa ya uchunguzi wa kifo cha marehemu.

"Ni kweli anashikiliwa na jeshi letu baada ya kupatikana malalamiko kutoka kwa baadhi ya ndugu kuwa mtuhumiwa alimpiga mfanyakazi huyo anayejulikana kwa jina la Vicent Siriri mwenye umri wa miaka 19 hivyo kilichofanyika mpaka sasa ni kumhoji mtuhumiwa," alisema.

Kamanda Shilogile, pia alieleza kuwa taarifa za awali zilidai kuwa marehemu alilazwa Hospitali ya Ilala kwa ajili ya matibabu ya Malaria hatua inayoongeza utata wa kifo cha marehemu Vicent.

Kutokana na mkanganyiko wa taarifa hizo, alisema kuwa kinachosubiriwa kwa sasa ni taarifa ya uchunguzi wa kifo cha marehemu kutoka kwa daktari ambayo ndiyo itathibitisha sababu za kifo chake.

"Marehemu alilazwa siku ya Jumanne na akafariki siku ya Jumatano na inadaiwa alikuwa akisumbuliwa na Malaria lakini baada ya kufa ndugu walidai kuwa marehemu alipigwa na mtuhumiwa hivyo tunachosubiri ni taarifa ya kifo kutoka kwa daktari ili hatua zingine ziendelee," alisema.

Hata hivyo taarifa zilizolifikia Majira kutoka katika eneo analoishi mtuhumiwa huyo, zilidai kuwa marehemu alikuwa ni mfanyakazi wake wa dukani ambapo inadaiwa kumpiga baada ya kupata hasara dukani na kisha kumkimbiza hospitali.

No comments:

Post a Comment