05 May 2011

Marekani yashinikizwa kuonesha picha za Osama

*Yadai bado inapima faida na hasara zake
*Wanasa kompyuta zenye siri za Al Qaeda


WASHINGTON,Marekani

UTATA juu ya mauaji ya aliyekuwa kiongozi wa kundi la kigaidi la Al Qaeda Bw. Osama bin Laden umezidi kutanda huku yakiibuka
maswali mengi kilichosababisha hadi kiongozi huyo auawe.

Mkanganyiko huo uliibuka juzi baada ya Ikulu ya Marekani (White House) kusema kuwa Bin Laden hakuwa amejihami wakati alipouawa na majeshi ya Marekani Jumapili iliyopita nchini Pakistan anakodaiwa kuwa amejificha kwa miaka kadhaa baada ya kukataa kukamatwa, huku ikitangaza kuwa itaanza kufanya uchunguzi ili kuangalia kama Pakistan ilikuwa ikimsaidia kiongozi huyo ambaye alikuwa akisakwa kwa muda wa miaka kumi.

Hadi jana Pakistan ilikuwa ikishikizwa zaidi kimataifa ikihojiwa ni vipi mtu huyo ambaye alikuwa akisakwa kwa udi na uvumba, aliweza kuishi karibu na kituo cha mafunzo ya kijeshi cha Abbottabad, Kaskazini mwa mji wa Islamabad, hali ambayo imevilazimu vyombo vya habari kutaka nchi hiyo ichukukuliwe hatua.


Mvutano wa vyombo vya usalama


Taarifa hizo za kwamba Bw. bin Laden hakuwa na silaha zinadiwa pia kuzua mvutano ndani ya vyombo vya usalama vya Marekani wa kwamba kutokana na kuwa kuna maswali yanayohoji ni jinsi gani kiongozi huyo wa al Qaeda alihusika katika majibizano ya risasi dhidi ya makomandoo walioshuka kwenye helkopta za Marekani.

Msemaji wa White House, Bw. Jay Carney juzi lizifananisha taarifa hizo kama 'ukungu wa vita', maneno ambayo waandishi waliyaita ni taarifa za awali za upotoshaji.


Uhusiano Marekani, mataifa ya Kiarabu


Inaelezwa kuwa endapo taarifa hizo zitabainika kuwa ni za kweli huenda zikakwamisha jitihada za Marekani kurejesha ushirikiano wake na mataifa ya Kiarabu duniani katika kumaliza mgogoro wa kivita katika nchi za Irak na Afghanistan ambao uliosababishwa na shambulizi la Septemba 11, 2001 ambalo linadaiwa kuandaliwa na Bin Laden.

Mbali na mtafaruku kuhusu taarifa hizo, inadaiwa kuwa vilevile maofisa wa Marekani bado wanashikana mashati kama waoneshe picha za mwili wa Bin Laden alivyopigwa risasi usoni, jambo ambalo litathibitisha kuhusu kifo hicho ingawa huenda likazua shutuma kutoka kwa Waislamu.

"Ni sahihi kusema kuwa picha hizo zinatisha," alisema Bw. Carney.


Kompyuta zenye siri za al Qaeda


Wachunguzi wa Marekani wanachunguza nyaraka na vifaa vya kompyuta walivyovikuta ndani ya jengo alimokuwa akiishi kiongozi huyo wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda, wakiwa na matumaini ya kuwa huenda wakapata taarifa nyeti kuhusu oparesheni za kundi hilo.

Bw. John Brennan, ambaye ni mkuu wa kitengo cha cha White House cha kupambana na ugaidi alisema jana kuwa wachunguzi hao vilevile wanafanya uchunguzi kwa vifaa hivyo ili kupata ushahidi ambao wanadhani utathibitisha kuwa maofisa wa serikali ya Pakistan walikuwa wakitoa msaada kwa kiongozi huyo wa al-Qaeda.

"Wanajaribu kujiridhisha kuona kama ama kuna mahusiano binafsi ndani ya Serikali ya Pakistan au maofisa usalama ambao walifahamu kuhusu kuwepo kwa makazi ya bin Laden au walikuwa wakitoa msaada," alisema Bw. Brennan.

"Tunaendelea kuangalia kwa makini taarifa hizo, tupo njiani kuwabaini viongozi wengine wa al-Qaeda," alisema mkuu huyo wa kitengo hicho kabla ya kusema kuwa inavyoonekana ni wazi kuwa kuna mtandao ambao ulikuwa ukitoa msaada na kusambaza taarifa kati ya Bin Laden na washirika wake.


Pakistan nayo yaanza uchunguzi


Kwa upande wake, Pakistan imeanza uchunguzi wa ndani kwa jinsi gani Bin Laden aliweza kuishi katika eneo hilo lisilokuwa na usumbufu akiwa na majenerali wastaafu wa jeshi.

Rais wa nchi hiyo, Bw. Asif Zardari anakataa shutuma za kuwa nchi yake  ibahifadhi makundi ya wapiganaji.

"Shutuma hizo zisizokuwa za msingi zinaweza kusambaa kwenye vyombo vya habari lakini taarifa hizo haziwezi kudhihirisha ukweli wa ni kwa nini Pakistan iwaelekeze wapiganaji wa Al Qaeda kwa taifa lolote," alisema Bw. Zardari.

"Vita dhidi ya ugaidi ni kubwa mno kwa Pakistan kama ilivyo kwa Marekani," aliongeza.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan naye vilevile alitoa taarifa akisema kuwa hakuwa na ufahamu wowote kuhusu operesheni ya Marekani dhidi ya Bin Laden na akasema kuwa Marekani ilikuwa ikiwatumia makachero wa nchi hiyo ambao iliwapatia miaka sita iliyopita ili kumsaka Bin Laden.

Bin Laden, mwenye umri wa 54, ambaye aliuawa Jumapili na majeshi ya Marekani alikuwa mwanzilishi na kiongozi wa kundi la al-Qaeda.

Inaaminika ndiye aliyeamru mashambulizi yaliyotokea mjini New York na Washington Septemba 11, 2001, pamoja na mashambulizi mengine ambayo yamekuwa yakisababisha vifo vya maelfu ya watu.

4 comments:

  1. Hivi watoe picha za mtu aliyeuwa kinyama akiwa kitandani pake uchi wa mnyama na mkewe? Mna akili kweli nyie???

    ReplyDelete
  2. NI VYEMA IKAWA WAZI DUNIANI IKAFAHAMU KWAMBA OSAMA AMEUWAWA KWA KUONYESHA MWILI WAKE NA SIO KUTUPIGA STORY 2, ISIWE KAMA MAMBO YA BALALI

    ReplyDelete
  3. Picha zote tunazoziona kwani cha ajabu ni nn? wameeleza alikamatwa na makomandoo wa marekani kabla ya kumuua, uliambiwa alikuwa kitandani?

    ReplyDelete
  4. SASA MAREKANI MTU WALIOKUA WANAMTAKA WAMEMPATA,YA NINI KUANZA KUISAKAMA NCHI? KWANI VIONGOZI WA NCHI WANAWEZA KUJUA KILA AINGIAE NA KUTOKA? MAANA KUNA WATU WENGINE HAWAPITII MIGRATION.ILA KUHUSU PICHA ITABIDI WATUONYESHE,TENA SIO PICHA TU MAANA KUNA PROGRAM ZA KUTENGENEZA PICHA NA KUONGOPEA WATU.WAMAREKANI WATUONYESHE VIDEO.

    ReplyDelete