*Vilio vya ndugu vyatanda mahakamani
Na Rehema Mohamed
VILIO na huzuni vilitawala katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana baada ya mahakama hiyo kutoa hukumu ya kifungo cha jumla ya miaka 21 jela
kwa watuhumiwa wawili wa kwanza wa kesi za wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Pamoja na hukumu hiyo, watuhumiwa hao, Mweka Hazina wa (CCM) Mkoa wa Kigoma Bw.Rajabu Maranda (53) na mpwa wake Bw.Farijala Hussein wametakiwa kulipa sh. bilioni 1.8 walichojipatia kwa njia ya udanganyifu kutoka BoT na kama watashindwa kufanya hivyo watafilisiwa mali zao.
Hukumu hiyo ilitolewa na jopo la mahakimu Bw. Saul Kinemela, Bw. Focus Bambikya na Bw. Elvin Mugeta, waliokuwa wakiisikiliza tangu awali, huku upande wa mashtaka ukiongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Mashitaka, Bw.Stanslaus Boniface na upande wa utetezi ukiwakilishwa na wakili wa kujitegemea Bw. Majura Magafu.
Watuhumiwa hao walikuwa wanakabiliwa na makosa manane na kupatikana na hatia katika makosa sita ambayo yalikuwa na hukumu ya kwenda jela kati ya miaka miwili na mitano.
Hakimu Bw. Mgeta akisoma hukumu hiyo alisema adhabu hizo za kutumikia kifungo zinakwenda kwa pamoja hivyo watuhumiwa watakaa jela miaka mitano ambacho ni kiwango cha juu kulingana na makosa yao.
Kabla ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Mwendesha Mashitaka alisema upande wa Jamhuri umeridhishwa na mwenendo wa kesi, hivyo mahakama ina kila sababu ya kutoa adhabu kali hasa ikizingatiwa kiasi cha fedha walichoiba watuhumiwa ni kikubwa na madhara waliyopata wananchi kutokana na kuibwa kwa fedha hizo.
Bw. Boniface aliiomba mahakama hiyo kwa mamlaka iliyonayo kutoa amri kwa watuhumiwa kurudisha fedha walizochukua kwa Jamhuri.
"Kwa sababu ni mara ya kwanza kwa watuhumiwa hawa kutiwa hatiani, hivyo naiomba mahakama ione kuwa ipo kila haja ya kutoa adhabu kali ukilinganisha kiasi cha fedha walichochukuwa, madhara waliyopata wananchi na pia fedha hizo wazirudishe kwa Jamhuri," alisema Bw. Stanslaus.
Hata hivyo, Wakili wa watuhumiwa hao, Bw. Magafu alipingana na upande wa Jamhuri akitaka watuhumiwa hao wasilipe fedha hizo kwa kuwa makosa wanayokabiliwa nayo hayapo chini ya kifungu cha sheria namba 358 cha makosa ya jinai, jambo ambalo lilipingwa vikali na upande wa jamhuri.
Bw. Magafu aliendelea kuwatetea wateja wake kuwa mahakama isitoe adhabu kali dhidi yao kwa kuwa ni kosa lao la kwanza na pia wanategemewa na familia zao.
Aliiambia mahakama kuwa mazingira ya makosa waliyotiwa hatiani mengi yalifanyika kwa kutojua ama kwa uzembe wa upande husika na kutolea mfano kuwapo kwa hati ya kuhamishia mali iliyopokelewa BoT na kuidhinisha fedha hizo.
Aliongeza kuwa watuhumiwa wote ni wagonjwa wanasumbuliwa na matatizo ya figo, hivyo iangalie pia kifungu cha sheria namba 138 cha kanuni ya adhabu ili iwaachie huru kwa masharti kuwa wasifanye kosa lolote kwa kipindi fulani.
Hata hivyo, Hakimu Mgeta wakati akisoma hukumu hiyo alisema mahakama imezingatia maombi ya pande zote mbili pamoja na uzito wa kosa na kuwa miongoni mwa adhabu zinazotolewa ni kuwaonywa kwa watuhumiwa hao.
Bw. Mgeta alisema pamoja na kutolewa kwa adhabu hizo haki ya kukata rufaa kwa watuhumiwa wote ipo wazi na wanaweza kufanya hivyo.
Baada ya hukumu, Bw. Magafu alisema tayari amezungumza na wateja wake na walimwambia kuwa hawajaridhika na hukumu hiyo hivyo wamemuomba afanye taratibu za kukata rufaa.
Bw. Magafu alisema kuwa hatua hiyo inaweza kuchukuliwa lakini kwanza ataomba mahakama hiyo impe hati ya hukumu ili aipitie kuangalia kama kuna uwezekano wa kukata rufaa ama la.
"Hukumu ilikuwa ndefu sana, wateja wangu wamenieleza nikate rufaa lakini kabla sijafanya hivyo itabidi nisome hukumu kwanza," alisema.
Kesi hiyo ni moja kati ya kesi za EPA zilizofunguliwa mfululizo Novemba 4 mwaka 2008 na upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi tisa ingawa mwanzo wa ushahidi, upande huo ulidai kuwa na mashahidi 22.
Washitakiwa hao wanadaiwa kula njama, kughushi, kuhusika katika wizi, kuwasilisha hati za uongo na kujipatia ingizo la fedha zaidi ya sh bilioni 1.8 katika akaunti yao kwa udanganyifu.
Inadaiwa kuwa fedha hizo mali ya BoT ziliingizwa kwa washtakiwa wakijaribu kuonesha kuwa kampuni yao ya Kiloloma Brothers imepewa idhini ya kukusanya deni la kampuni ya BC Cars Export ya Mumbai, India lililokuwa BoT.
Pamoja na hukumu hiyo, Bw. Maranda anakabiliwa na kesi nyingine nne za aina hiyo katika mahakama hiyo, wakati Bw. Farijala anakabiliwa na kesi tatu za aina hiyo na wote wako nje kwa dhamana.
No comments:
Post a Comment