18 May 2011

Ajali yaua 16 Geita

*Wengine 58 wajeruhiwa

Na Faida Muyomba, Geita

SIMANZI na vilio vimetanda katika Kijiji cha Chibingo, wilayani Geita, baada ya watu 16 kufa papo na wengine 58 kujeruhiwa vibaya baada ya mabasi
mawili ya abiria kugongana uso kwa uso.

Ajali hiyo ambayo ilitokea jana mnamo saa 3.30 asubuhi ni ya basi la Sheraton lenye namba za usajili T. 268 AJC mali ya Bw. Talib K. Abdallah na lile la Bunda lenye namba T. 810 BDW.

Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Bw. Philemon Shelutete alisema kuwa watu 12 walikufa papo hapo na wengine watatu walifariki dunia katika Hospitali ya Wilaya ya Geita.

Alisema hali za majeruhi zilikuwa mbaya na kulikuwa na uwezekano wa vifo kuongezeka.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Geita, Dkt. Omari Dihega alithibitisha kupokea miili ya watu 15 pamoja na majeruhi 58 waliotokana na ajali hiyo.

Taarifa ya Jeshi la Polisi mkoani mwanza iliyotufikia wakati tunakwenda mitamboni ilisema idadi ya waliokufa ilikuwa imeongezeka hadi kufikia 16. Kati yao watu wazima ni 14 na watoto ni 2. Maiti 6 zilikuwa zimetambuliwa huku majeruhi waliokuwa wamesalia hospitali walikuwa 48 baada ya wengine kutibiwa na kuruhusiwa.

Majina ya watu waliokufa yalikuwa hayajafahamika taarifa zaidi zilisema  kuwa huenda miongoni mwa waliokufa yumo askari wa polisi kutokana na kuokokwa kwa kofia yake.

Alisema, hali za majeruhi ambao wamelazwa hospitalini hapo ni mbaya na kwamba majeruhi saba wamehamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi.

Alisema miongoni mwa majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo yumo mtoto mchanga Amina Abdallah, mwenye umri wa wiki tatu ambaye alinusurika na bila jereha lolote licha ya kupatwa na maumivu kiasi mwilini.

Aliwataja baadhi ya majeruhi ambao walihamishiwa Bugando kuwa ni pamoja na Bw. Boniphace Kitogoro (46), Bw. Joseph Mabubaga(32), Bi. Lulu Ishabakaki (30), Bi. Florentina Magoge (32) pamoja na Bi. Lucia Edmund (8).

Wakizungumza na waandishi habari eneo la tukio, baadhi ya watu walioshuhudia ajali hiyo walisema, ilitokana na basi la Shereton kutaka kulipita gari jingine aina ya Fuso lenye namba T. 823 BPV, yote yakitoka Ushirombo kwenda Mwanza na kugongana na basi la Bunda lililokuwa likitoka Mwanza kwenda Karagwe, mkoani Kagera.

No comments:

Post a Comment