Na Mwandishi Wetu
KIKOSI cha ukusanyaji masalia ya milipuko ya mabomu kwa kushirikiana na maofisa wa Marekani, leo wataanza kulipua masalia ya mabomu katika kambi ya Gongolamboto, Dar es Salaam, kuanzia saa moja asubuhi hadi saa sita mchana.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Kurugenzi ya Habari na Mawasiliano Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), imesema kazi ya kulipua masalia hayo itafanyika kwa wiki moja hadi Mei 11, mwaka huu.
Mabomu hayo yatalipuliwa ndani ya kambi hiyo kutokana na hatari kubwa inayoweza kutokea wakati ya kuyabeba na kuyapeleka maeneo ya mbali ili yaweze kulipuliwa.
“Masalia mengine yatalipuliwa baadaye huko Msata, Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani, tunawaomba wananchi waishio maeneo karibu na kambi, wakazi wa Dar es Salaam na vitongoji vyake, kuwa watulivu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Februari 16, mwaka huu mabumu yalilipyka katika maghala kwenye kambi ya Gongolamboto na kusababisha vifo vya watu 27 na wengine zaidi ya 300 kujeruhiwa, huku wengine wakikosa makazi.
No comments:
Post a Comment