Na Mwandishi Wetu
WAMILIKI wa mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani wamewaomba radhi abiria kutokana na usumbufu walioupata juzi iliyopita uliosababishwa na mgomo wa
baadhi ya madereva.
Wamiliki hao katika taarifa yao wamesema watawachukulia hatua za kisheria madereva waliohusika kushawishi mgomo na ambao wengine hawana mabasi wanayoendesha.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Dar es Salaam (DABOA), Severine Ngallo alisema mgomo uliotokea Jumapili ulisababisha adha kubwa kwa wasafiri, ndugu na jamaa zao, hivyo wanaomba radhi na kuahidi kuwa hali hiyo haitatokea tena.
“Tungejua kuwa madereva wetu wamepanga kugoma, tusingukubali kukatisha tiketi na kusababisha usumbufu kwa abiria, kama walipanga kugoma wasingechukua mabasi nyumbani au gereji na kuyapeleka stendi, kilichofanyika ni uhuni,” alisema Ngallo.
Aliongeza kuwa: “Kuna genge la baadhi ya madereva lililoshurutisha kufanyika kwa mgomo huo na ndiyo maana waliwapiga baadhi ya madereva waliokataa kushiriki mgomo. Haukuwa mgomo wa madereva wote ndiyo maana baadhi ya mabasi tayari yalikuwa yameingia kwenye foleni ya kutoka.”
Wamiliki hao kutoka mikoa mbalimbali nchini waliokutana jana mjini Dar es Saaam waliazimia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika na kuwa suala la mkataba kati ya mmiliki na dereva ni mambo binafsi kwani hata mishahara inatofautiana kutokana na makubaliano yaliyofikiwa.
Katika hatua nyingine, mkutano wa wamiliki hao ulikuwa ukiendelea jana jioni ambapo wamiliki hao walikuwa wakijadili kuhusu mgomo kupinga kufungwa kwa mfumo wa udhibiti mwendo.
Habari zilizopatkana wakati mkutano huo ukiendelea zilisema wamiliki hao watamuona Waziri wa Uchukuzi, Bw. Omari Nundu kabla ya kuanza rasmi mgomo huo ili kuepuka kukurupuka katika kuchukua maamuzi waliyokusudia.
“Bado tunaendelea na kikao baada ya mapumziko ya mchana, mgomo upo palepale, lakini kabla ya kuufanya itabidi tuonane na waziri mwenye dhamana,” alisema mmoja wa wamiliki hao ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
No comments:
Post a Comment