Na Masau Bwire, Bagamoyo
MAJAMBAZI zaidi ya 10 yaliyokuwa na bunduki moja na silaha nyingine za jadi wamefunga barabara ya Msata-Bagamoyo kisha kuwapora fedha na mali, kuwavua
nguo baadhi ya abiria baada ya kulaza magogo na mawe makubwa barabarani, eneo la Kitongoji cha Changa, kata ya Msata.
Tukio hilo lilifanyika Jumapili majira ya saa 1:15 jioni na kudumu kwa dakika 45 ambapo, ambapo abiria waliwekwa chini ya ulinzi na kushushwa kwenye magari yao na kulazwa chini ndani ya madimbwi ya maji na tope kisha, kuamriwa kutoa mali zote na fedha na kuzikabidhi kwa majambazi, huku wale waliodai hawana chochote wakivuliwa nguo na kubaki 'uchi wa mnyama'.
Akizungumza jana na gazeti hili, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Msata, Bw. Edgar Nazar alisema majambazi hao walipora mali mbalimbali za abiria hao ambazo thamani yake halisi bado haijafahamika zikiwemo fedha taslimu na simu za mkononi.
Bw. Nazar aliwataja baadhi ya waathirika kuwa ni pamoja na Bw. Semeni Issa, mkazi wa Msata aliyekuwa akiendesha gari lenye namba za usajili T 985 ANV Toyota Corola akitoka Bagamoyo kwenda Msata akiwa na abiria sita ambaye kwanza alitulizwa kwa kupigwa na ubapa wa panga kichwani kisha kuporwa simu ya mkononi na sh. 45,000.
Alisema miongoni mwa abiria wa Bw. Issa alikuwa ni Daktari wa Kituo cha Afya Chalinze, Victor Bamba na mkewe ambao waligalagazwa kwenye tope kisha kuamriwa wakabidhi kila walichokuwanacho kwa majambazi hao ambapo, Dkt. Bamba alikabidhi fedha na simu ya mkononi na mkewe akadai hana mali yoyote.
Baada ya mwanamke huyo kudai hana mali yoyote aliamriwa na majambazi hao kuvua nguo zake zote, na alipovua alikutwa ameficha simu mbili na sh. 40,000 kwenye nguo za ndani na kuonywa kwa kupigwa na ubapa wa panga katika makalio yake na kuelezwa kwamba siku zote anapaswa awe mwaminifu, asifiche 'mali za watu' mbali kiasi hicho.
Katika hatua kuwavua nguo abiria waliodai hawana fedha, simu wala mali nyingine, mwanamke mmoja alibainika hakuwa na chochote lakini akakutwa amevaa shanga nyingi kiunoni, alipotakiwa na majambazi hao kueleza kazi za shanga hizo, alidai ni za dawa na majambazi hao wakazikata kwa panga na kumtandika nalo kwenye makalio, kisha kumtaka asirudie kuzivaa wakati hana fedha.
Baadhi ya magari yalifanikiwa kugeuza na kurudi yalikokuwa yakitokea kabla ya kufika eneo la tukio na kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama ambapo, askari wa Kampuni ya Ujenzi ya Espem inayojenga barabara ya Bagamoyo-Msata walikuwa wa kwanza kufika eneo hilo lakini, majambazi hao wakawa tayari wametokomea vichakani.
Hata hivyo kwa ushirikiano wa uongozi wa kata ya Msata, tarafa na polisi mkoani Pwani, msako mkali uliendeshwa na kumkamata Bw. Isiaka Kichwa (21), mkazi wa Msata ambaye anadaiwa wakati uporaji huo ukiendelea yeye, alikuwa mjini Msata, njia panda ya Tanga akifanya mawasiliano na waporaji kuhusu hali ya usalama wao na kuwajulisha kama askari wanaelekea eneo la tukio.
Jeshi la polisi mkoani Pwani limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kwamba, lipo katika msako mkali kuhakikisha wote waliohusika katika tukio hilo wanakamatwa na kufikishwa mahakamani.
nahisi hao ni wanajeshi kwa jinsi mbinu waliyotumia na walivyofanya uporaji, kama kugaragaza watu kwenye matope.
ReplyDeletemasau bwire nipigie simu namba 0715933308 au 0754933308 ninakuhitaji kwa mazungumzo
ReplyDeleteHivi kudhalilisha binaadamu wenzako unapata faida gani?
ReplyDeleteJamani kuweni na ubinaadamu hata kama ni jambazi, angekuwa mke wako au mama yako ungekubali kufanyiwa vitendo hivyo?
Kuna siku Mwenyezi Mungu atawaadhirisha nyinyi.
Tatizo ni kuwa,hata majambazi wakikamatwa wanafungwa kwa kipindi cha muda mfupi halafu wanaachiwa,au wengine wanatoka kwa hongo.Laiti kama sheria za kiislam[mwizi akatwe mkono,akiiba tena hali kadhalika] zingekuwa zinachukua mkondo wake nafikiri mambo ya wizi na ujambazi vingepungua sana kama si kuisha kabisa
ReplyDeleteMtindo huu wa ujambazi unazidi kusogea ulianzia huko mikoa ya magaharibi na lawama nyingi tukawapa wakimbizi wa kirundi, lakini je ni kweli? jeshi la Polisi lijipange vizuri kudhibiti ujambazi wa aina hii suala la shanga linaingiaje? je mpaka sasa wamekamatwa hao wahalifu?
ReplyDelete